Wednesday, November 12, 2008

Ivo bado yupo Stars
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa 'Taifa Stars', Mbrazili Marcio Maximo amemuita kipa Ivo Mapunda kwenye kikosi chake cha wachezaji 27 kinachojiandaa na mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Msumbiji wiki ijayo.

Pia kikosi hicho ndicho kitakachoikabili Sudan katika mchezo wa kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani utakaofanyika Novemba 29 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Ivo ameitwa katika kikosi hicho, ingawa amefuzu majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika timu ya St.Georges ya Ethiopia, lakini hadi sasa ameshindwa kujiunga kutokana na kutopata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC), baada ya Ethiopia kufungiwa kwa muda usiojulikana na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Mapema mwezi uliopita Maximo alikaririwa akisema kuwa kutokana na Ivo kuondoka, angepoteza sifa ya kucheza mechi dhidi ya Sudani, hivyo alikuwa akiwaandaa Farouk Ramadhani na Shaaban Dihile, Deo Munisi ili kuchukua nafasi ya Ivo, ambaye amekuwa chaguo la kwanza la Mbrazili huyo tangu aje nchini Julai 2006.

Akitangaza kikosi hicho jana, Maximo, alisema uwezo nidhamu na juhudi za wachezaji walioitwa ndiyo vilivyowapa nafasi na kusema ataendelea kufanya hivyo kwa wachezaji wote watakaokuwa na sifa hizo.

Hata hivyo katika kikosi hicho, hakuna sura mpya, badala yake wengi wao ni wale wale ambao walikuwepo kwenye kikosi kilichoifunga Cape Verde mabao 3-1 katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2010 Septemba mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji walioitwa tena licha ya Mapunda ni Dihile, Farouk Ramadhan, Deo Munishi, Shadrack Nsajigwa, Nurdin Bakari, Kelvin Yondan, Omar Bakari, Salum Suedi, Nadir Haroub, Meshack Abel, Juma Jabu, Amir Maftah, Henry Joseph na Geofrey Bonny.

Wengine ni Athuman Idd, Shaaban Nditi, Abdi Kassim, Haruna Moshi, Nizar Khalfan, Kigi Makasi, Jabir Aziz, Uhuru Seleman, Mrisho Ngassa, Mussa Hassan, Jerry Tegete na Moses Godwin.

SOURCE: Majira

No comments: