Saturday, November 14, 2009

Kila la heri Baraza
KLABU ya Yanga imeamua kuachana na mshambuliaji wa Kenya, Mike Baraza na imemtakia kila la heri anapokwenda.

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Yanga mtaa wa Twiga na Jangwani jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu amekiri kumalizika mkataba na mchezaji huyo, ingawa bado walikuwa wanamhitaji. “Mkataba wetu na Baraza kweli umekwisha na bado tulikuwa tunamhitaji ndio maana tumekuwa tukijaribu kuwasiliana naye ili tufanye mazungumzo, lakini hakuleta ushirikiano hivyo tunamtakia kila la heri huko aendapo.


“Lakini hajafanya vizuri kwa sababu yeye ni mchezaji huru, angekuja tufanye mazungumzo kama angekuwa hataki kurudi tena Yanga si angesema sisi tunamtakia kila la heri licha ya kutoonesha uungwana hakatazwi kwenda kokote,” amesema Sendeu.


Mwanzoni mwa wiki hii mchezaji huyo aliripotiwa kuingia mkataba na Simba ya Dar es Salaam, ambayo ni mpinzani wa jadi na Yanga. Sendeu amesema, nafasi ya Baraza itachukuliwa na John Njoroge aliyekatwa kwenye usajili baada ya Ligi Kuu kuanza. TFF iliitaka Yanga kuondoa jina moja kati ya majina 11 ya wachezaji wa kigeni iliowasajili, ili nafasi hiyo ichukuliwe na George Owino ambaye alihalalishwa kuichezea timu hiyo.


Kuhusu usajili wa dirisha dogo, Sendeu alisema bado kocha Kostadian Papic anaendelea na suala hilo na jana alitarajiwa kumjaribu Sergie Okwundu kutoka Abuja FC ya Nigeria. “Pia anaendelea kumuangalia Salvatory Edward, amemwambia aendelee kuja mazoezini aone kama anaweza kumchukua ama vipi,” alisema.


Alisema pia wamemuuza kwa mkopo Vicent Barnabas kwenda African Lyon atakapocheza kwa miezi sita. “Tutaendelea kumsikiliza kocha nani anamhitaji na nani hamhitaji…tutaendelea kuwauza kwa mkopo ili kupata nafasi ya kusajili wengine,” alisema Sendeu.


Pia alisema baada ya mechi ya keshokutwa dhidi ya Prisons wachezaji watapewa mapumziko ya siku kumi na kwamba kocha Papic atakwenda kwao Serbia kuchukua familia yake.

HABARI LEO

No comments: