Wednesday, June 30, 2010

Kifukwe atemwa Yanga


Kamati ya uchaguzi ya Yanga chini ya Jaji mstaafu John Mkwawa imewapiga chini kuwania uongozi ndani ya klabu hiyo Francis Kifukwe, Hashimu Lundenga na Hassan Mwanakatwe kutokana kile kilichotanabahishwa kama kukosa sifa za uongozi.

Kamati hiyo iliyokaa usiku wa kuamkia leo pia imemchinjia baharini tajiri Abeid Abeid 'Falcon' kutokana na kushindwa kuwasilisha vyeti halisi vya shule.

Akizungumza makao makuu ya klabu hiyo leo hii, Ofisa habari wa Yanga, Louis Sendeu kasema Kifukwe ambaye alipewa nafasi kubwa kutokana na kukubalika kwa wanachama na swahiba mkubwa wa mfadhili wao Yusuf Manji alienguliwa baada ya kutotokea kwenye
usaili.

"Kifukwe aliwekewa pingamizi hivyo alitakiwa kufika kwenye usahili ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili za kuuza basi wakati wa uongozi wake lakini hakutokea hivyo kamati imemuengua kwenye kinyang'anyiro cha wagombea."alisema Sendeu.

Sendeu alisema pingamizi lililokuwa likimkabili Lundenga ambalo limesababisha kuondolewa kwenye kinyang'anyiro hicho baada ya kutoa utetezi ambao haujajitosheleza ni wakati wa uongozi wa Iman Madega ambao umemaliza muda wake alikuwa ni mjumbe wa kamati ya utendaji hivyo alishindwa kumshauri vema mwenyekiti kuitisha mkutano na kuweka wazi mapato na matumizi tangu uongozi huo ulivyoingia madarakani mwaka 2006.

Pia Lundenga aliambiwa kuwa alishindwa kumshawishi Madega wasiiondoe timu kwenye michuano ya Kombe la Kagame mwaka juzi 2008 ambao Yanga waligomea mechi kati yao na Simba ya kuwania mshindi wa tatu kwenye michuano hiyo na hivyo kusababisha kufungiwa
kushiriki michuano hiyo ya Kombe la Kagame kwa muda wa miaka
miwili ikiwa ni pamoja na kulipa faini ya dola 35,000.

Hassan Mwanakatwe nae pia alikuwa mjumbe wa kamati ya utendaji kwenye uongozi wa Madega nae alikabiliwa na tuhuma kama za Lundenga.

Kwa maamuzi hayo watakaowania nafasi ya mwenyekiti anayepewa nafasi kubwa baada ya kung'olewa Kifukwe ni wakili Lyoid Nchunga ambaye pia aliwekewa pingamizi la uraia hata hivyo Sendeu alisema Nchunga aliwasilisha vyeti vyake halisi vya kuzaliwa ikiwa ni pamoja na hati ya kusafiria hivyo rufaa iliyokatwa dhidi yake imetupwa.

Hivyo Nchunga hivi sasa atachuana na Mbaraka Igangula, na mwalimu wa Makongo Edgar Chibura wakati kwa upande wa Makamu mwenyekiti ni watakaochuana ni Constatine Maligo, Ayoub Nyenza na David Mosha ambaye anapewa pia nafasi kubwa ya kuibuka kidedea kwenye kinyang'anyiro hicho.

Wanaowania nafasi ya ujumbe kati ya wagombea 30 wagombea 29 wamepita na mgombea mmoja David Mkangwa ameenguliwa kutokana na kushindwa kutokea kwenye usaili.

Sendeu alisema kuanzia Julai 2 hadi 5 ni kipindi cha pingamizi na atakayekata atalazimika kulipa shilingi 500,000 wakati kampeni zimepangwa kuanza rasmi Julai 7 hadi 12 huku uchaguzi mkuu umepangwa kufanyika Julai 18.

No comments: