Saturday, February 05, 2011

Sam TImbe kocha mpya Yanga
HATIMAYE klabu ya Yanga, imemtambulisha kocha mpya, Sam Timbe kuziba nafasi ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Kosta Papic aliyetimkia kwao baada ya migogoro ya hapa na pale ndani ya klabu hiyo.

Kocha huyo alitambulishwa jana kwa waandishi wa habari ofisini kwa mfadhili mkuu wa timu hiyo, Yusuf Manji jengo la Quality Plaza, Barabara ya Nyerere. Hata hivyo, alisema kuwa hajamalizana na Yanga kuinoa timu hiyo.

"Najua kuna mpasuko Yanga, viongozi hawaelewani, naomba tuwe marafiki tushirikiane, viongozi, wachezaji na mashabiki kwa ajili ya maendeleo ya Yanga, bila hivyo timu haiwezi kufanya vizuri," alisema Timbe.

Sam Timbe aliyeziongoza SC Villa na Polisi na kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati michuano iliyofanyika Tanzania mara zote, ataanza kuinoa timu hiyo kwa majaribio kabla ya kupewa mkataba wake.

Timbe alisema bado hawajamaliza na uongozi wa Yanga kuhusu mkataba wake na ameondoka jana kurudi Uganda na anatarajia kurejea nchini Jumapili na kuongoza jahazi la timu hiyo.

Kocha huyo wa Atraco alikuwa na ndoto kubwa za kunoa timu za Tanzania hususani Simba na Yanga na alidai kuwa bado anafanya mazungumzo na anatarajia yataenda vizuri, na iwapo watafanikiwa kusaini mkataba habari za ndani zinadai kuwa atasaini wa mwaka mmoja.

1 comment:

Anonymous said...

jamani yanga imepata lulu! huyu anafaa kukochi hata taifa stars.good luck wanayanga wote.