Monday, May 21, 2007

Yanga moja kuelekea kwenye uchaguzi

Wanachama 349 jana kwa kauli moja walipitisha rasimu ya katiba ya mwaka 1992 na sasa Yanga ni moja kuelekea kwenye uchaguzi Mei 26.

Kwa hatua hiyo, sasa wanachama wote wa Yanga wanaweza kupiga kura bila kujali aina ya kadi anayotumia mwanachama.


Pia rasimu hiyo ya katiba, imepitishwa kuwa na Kampuni mpya ya Umma ya Young Africans Sports Club Corporation ambayo klabu itakuwa na umiliki wa 51%. Wanachama wa klabu hiyo watanunuliwa hisa na mfadhili wao Yusuf Manji mara tu kampuni hiyo itakapoanza mauzo ya hisa zake.


Aidha katika kwenda na wakati, kiwango cha ada pamoja na bei yz kadi mpya zimepanda ambapo sasa ada ya mwanzo ya 600/= kwa mwaka sasa itakuwa 12,000/= . Uanachama sasa ni 2000/= badala ya 500/=.


Rasimu hiyo ya katiba inatarajiwa kufikishwa kwa Msajili wa klabu na vyama vya michezo wa wilaya ya Ilala kwa ajili ya kusajiliwa.

Ni uamuzi wa busara uliofikiwa na wanachama. Tuombe Mungu mambo yabaki hivi kwa kipindi chote cha uchaguzi ili tuweze kupata uongozi wenye baraka za wanachama wote.

Mchakato wa uchaguzi wa Yanga ulikuwa umesimamishwa na ofisi ya michezo wilaya ya Ilala hadi hapo wanachama watakapokaa pamoja na kupitisha rasimu hiyo ya katiba. Kufuatia rasimu hiyo kupitishwa hapo jana, uchaguzi wa Yanga sasa utaendelea kama ulivyopangwa.

Yanga Imara, Daima mbele.

2 comments:

Anonymous said...

Hongereni wanaYanga kwa kuonesha ukomavu kimichezo. Mmeamua kuweka tofauti pembeni kwa manufaa ya Klabu. Kilichobaki sasa tuwe pamoja kuelekea uchaguzi, tuchague viongozi watakaoipeleka klabu na timu mbele zaidi. 'Mbele' simaanishi kwenye kuwafunga Simba, bali kwenye kutwaa ubingwa wa Afrika na pia kuwa na Klabu inayojiendesha kwa vitega uchumi vyake.

Kwa taarifa za magazeti, wanachama waliohakikiwa Dar kwa ajili ya uchaguzi ni kama 1,000 hivi na ushee. Lakini nadhani wapenzi wa Yanga ni mara mia zaidi ya hao ambao ni wanachama kwa sasa. Sasa wazo langu ni kuwa viongozi wapya watakaopatikana, wawe na mkakati wa kuongeza wanachama, toka 1000 wa Dar kwa sasa mpaka walau 600,000 kwa Dar pekee. Nadhani hili linawezekana. Ni mikakati tuu na uwezo na nia ya viongozi kutekeleza majukumu.

Shilingi 12,000 ada uanachama sii kubwa sama kuwashinda watu wengi, ingawa pia sio kidogo. Ni wastaniwa Sh. 1,000 kwa mwezi. Hapa viongozi wanaweza kuweka utaratibu wa watu kulipia kwa mwezi au kwa msimu (kama miezi 3 unalipa sh. 4,000). Waweke account ya Klabu (ama kampuni ya klabu) hadharani wanachama walipe moja kwa moja kwenye akaunti, badala ya kwenda klabuni kujipanga foleni na kumpa mtu ambaye huna uhakika kama anafikisha hela hizo klabuni ama mfukoni kwake...! Hii pia itasaidia wanachama waliopo mikoani na nje ya nchi.

Kuwe pia na incentives kwa wachama kulipia kadi zao kila mwaka, mfano wanaweza kusema wanachama waliolipia kadi zao wanapata T-Shirts na kofia za timu bure. Inawezekana kuzitoa T-Shirts bure kwa wanachama bila gharama kwa klabu kwa kutumia wadhamini/wafadhili kujitangaza kwenye hizo Souvenirs.

Kwa ajili ya transparency (uwazi), ni vizuri klabu iwe na website yake ambapo wanachama watakuwa na private access kuweza kuona mambo yanayoendelea na kucheki kwa mfano kama michango yote mtu alitoka imepokelewa ama bado kiasi gani n.k.

Wadau wengine mnaweza kuendelea na maoni/mawazo mengine. Bila shaka kama viongozi watarajiwa watapitia hapa wanaweza kudesa some implementable ideas.

JM.

CM said...

Kweli mawazo yako ni mazuri sana. Nakuunga mkono.

Naamini Yanga ina wapenzi wengi ambao wanatamani kuwa wanachama lakini wanakabiliwa na vikwazo kibao mpaka wanaona bora wawe mashabiki tu.

Ni vema ikapigwa kampeni ya kuwavuta mashabiki kuwa wanachama kiasi kwamba kwa kupitia michango yao mbalimbali, wataweza kuiimarisha klabu kimapato kwa kununua hisa n.k

Pia klabu kupitia hizo fedha inaweza kuanzisha miradi mbalimbali ikemo maduka pekee ya kuuza bidhaa kama kalenda, jezi, fulani, kofia, wheel covers n.k zenye nembo ya Yanga.

Tunapoelekea kwenye uchaguzi hivi sasa malengo yetu si ya kuweka mtu madarakani kwa vile tu 'ni kiboko ya Simba'. Ni lazima tuwe na focus ya mbali zaidi.

Ni hayo tu kwa sasa.