Saturday, May 26, 2012

Nchunga Ajiuzulu

Hatimaye Mwenyekiti wa Yanga mwanasheria Lloyd Nchunga ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi yake hiyo aliyokuwa anaishikilia baada ya kulalamikiwa na wanachama wa klabu hiyo kuwa ameshindwa kuwangoza.

Shinikizo lililomsukuma Nchunga kuachia madaraka hayo lilionekana kuzidi pale wanachama zaidi ya 700 walioongozwa na Baraza la Wazee walipokutana kwenye makao makuu ya klabu hiyo Jumapili iliyopita katika mkutano wa wanachama ambao haukuwa rasmi kwa mujibu wa katiba.

Ufuatao ni waraka wa kutangaza kujiuzulu kwa Mwenyekiti Lloyd Nchunga.

Ndugu wana Habari,

Najua kwamba taarifa hii itawafedhehesha wajumbe na wanayanga wanaotuunga mkono,hasa ukizingatia maamuzi ya pamoja ya vikao vyetu vya kamati ya utendaji vilivyopita kwamba hakuna wa kujiuzulu kati yetu mpaka tujue hatma ya mkutano mkuu ambao tulipanga ufanyike tarehe 15 Julai 2012, ukiachia mbali shinikizo la kujiuzulu linalotolewa na baadhi ya wazee na wanaojiita vijana wa klabu, kwa wajumbe wa kamati ya utendaji, na hasa mimi kama mwenyekiti.

Nawashukuru wajumbe kwamba tulifanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mzuri, na hata pale tulipotofautiana tulifanya hivyo kwa hoja na kufikia maazimio ambayo wote tulikuwa tunawajibika nayo.

Tangu tumeingia madarakani tumeweza kushirikiana na kupata mataji matatu katika kipindi cha mwaka mmoja, yaani; Ngao ya Hisani 2010, Ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom 2010/2011, na Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), 2011. Zaidi ni kwamba tuliuwa uteja kwa watani wetu wa jadi kila tulipokutana katika ligi ukiachia mbali mechi ya tarehe 6 Mei 2012, ambayo tulifungwa goli 5 bila, na kuleta mtafaruku mkubwa katika klabu yetu.

Hali kadhalika tumeshirikiana mpaka tumeweza kuboresha mkataba kati yetu na TBL kupitia Kilimanjaro Premium Lager, tumeingia mkataba na kampuni ya NEDCO kuendeleza mali zetu katika mtaa wa mafia na uwanja wetu wa KAUNDA baada ya kufikia hatua nzuri katika kupata hati miliki za maeneo yote mawili.

Nafahamu kwamba kampuni hiyo iko katika hatua za mwisho za kumalizia michoro. Hali kadhalika tuliingia mkataba wa kuzalisha na kuuza bidhaa zenye nembo yetu na hasa baada ya kufanya marekebisho yatokanayo na matakwa ya sheria kule BRELA na pia mkataba na kampuni ya NEXUS LTD, ambayo itakuwa inatutafutia wadhamini wa nje na ndani, kufanya promosheni zetu na kampeni kwa njia ya electronic kupitia mitandao mbalimbali na kukusanya data za wanachama na kusajili wapya tukiwa na malengo ya kukusanya shilingi 300,000,000/= hadi 800,000,000/= kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitatu. Haya yote tuliyafanya tukilenga kujitegemea kujazia mapengo yaliyokuwa yakitokana na kutegemea ufadhili wa mtu mmoja mmoja.

Kwa ridhaa yenu tumekua tukiendelea na mazungumzo na makampuni mbali mbali kwa ajili ya udhamini na kwa sababu maalum, nitazitaja katika hati ya makabidhiano kwa kiongozi ajaye.

Aidha, tumeshirikiana katika kufanya mambo mbali mbali ya kijamii, ikiwa ni pamoja na sikukuu ya kuadhimisha miaka 77 ya Yanga, sikukuu za pasaka, kuchangia jamii na waliokumbwa na maafa, na kongamano la vijana lililolenga kuwaamsha vijana kuitambua nafasi yao katika Yanga ikiwa ni pamoja na kupata azimio la kuanzisha SACCOSS ya Yanga, ambapo maombi yapo kwa msajili Manispaa ya Ilala.

Haya yote nayataja ikiwa ni kuwashukuru kwa ushirikiano na ikiwezekana muweze kuyakamilisha yaliyobaki ambayo mtaona yalikuwa mazuri. Lakini pia tulipopata matatizo tulikuwa pamoja. Nichelee kusema tu kwamba tulisimama pamoja baada ya kujiuzulu Makamu Mwenyekiti wetu Ndugu Davis Mosha na mjumbe wetu ndugu Seif A. Seif, Ali Mayayi, na wengineo, kwani tulifungwa na katiba.Tulisimama pamoja pia katika suala la kujiuzulu ndugu Yusuf M. Manji, aliyekuwa mdhamini mteule na mfadhili mkuu ambaye sasa ameonyesha nia ya kurudi nanyi mkaridhia mkutane naye.

Awali, tulitumia kila jitihada za kumrejesha lakini ikashindikana. Hata hivyo doa limetupata baada ya kufungwa na watani wetu goli 5 bila, ambapo kuna wanachama wanaoelewa na wasioelewa kabisa.

Ninachokiona mimi ni usaliti wa hali ya juu uliombatana na matukio mbalimbali yaliyopita na yanayoendelea hadi kujaribu kupindua uongozi wa halali wa kidemokrasia. SIWATUHUMU WACHEZAJI MOJA KWA MOJA, isipokuwa mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo ule na sasa, inaonyesha kwamba kulikuwa na usaliti mkubwa ambao sisi hatukuweza kuubaini mapema. Sioni mantiki katika hoja kwamba wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho n.k. Au ati mtendaji wetu alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli, ndiyo tuvune bao 5!

Kwa wanaoijua Yanga, imewahi kuwa na madeni makubwa katika Hoteli mbali mbali, mawakala wa ndege n.k, na baadhi tumeyakuta na sisi tumekuja tukayalipa. Hii imewahi kutokea kabla na wakati akiwepo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa baki, na bado wachezaji walicheza kwa morali.

Hata hivyo, utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatula kama hatutaiacha, kwani wenye hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuuondoa uongozi wa kidemokrasia. Baada ya mapinduzi kushindikana na TFF kuonya kuhusu mapinduzi hayo, wazee kupitia msemaji wao , Mzee Akilimali wamesikika katika kipindi cha Michezo cha Redio moja maarufu hapa nchini wakidai kwamba ni bora Yanga ishushwe daraja au kufungiwa kuliko mimi kuendelea kuongoza! Hii imenikumbusha HEKMA ZA MFALME SELEMANI akiamulia ugomvi wa wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto naye akaamuru wamgawane nusu kwa nusu. Yule mwenye mtoto kweli alimuomba Mfalme amuachie mwenzie kuliko kumkata nusu. Kwa hekma hiyo nimeamua kujiuzulu nafasi yangu katika Uenyekiti wa Yanga kwani ni klab ninayoipenda hata kama sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba yetu.

Vile vile siko tayari kuona klab yangu ikisalitiwa au kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni kiongozi. Natumaini kamati ya utendaji kwa pamoja na wale tuliowateua chini ya ibara ya 29(3) ya katiba ya Yanga pamoja na bodi ya wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka kufikia mkutano mkuu kwa mafanikio zaidi.

Nitaendelea kuwa mwanachama mwadilifu na nitatoa mchango wangu wa hali na mali pale nitakapo hitajika na nikiwa na uwezo wa kufanya hivyo.

YANGA DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO.

Wasalaam,

LLOYD NCHUNGA BIHARAGU.

Nakala kwa:-
Mama Fatma Karume,
Mdhamini Francis Kifukwe,
Mdhamini Bwana Yusuf Manji – Kwa taarifa

LLOYD NCHUNGA BIHARAGU
C/O LLOYD ADVOCATES,
Morogoro/Bibi TIti Mohamed Rd,
7th Floor, J.K. Nyerere Pension towers
P.O. BOX 75111,
Dar-Es- Salaam,
Tanzania.Tuesday, May 08, 2012

Ligi Kuu ya Vodacom

Simba bingwa

Simba imefanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom Tz baada ya kujikusanyia pointi 62. Katika mchezo wa mwisho wa ligi hiyo, Simba iliichapa Yanga 5-0 na kukabidhiwa kombe katika uwanja wa Taifa Jijini Dar.


Hongereni mabingwa.

Sunday, October 30, 2011

Simba achinjwaGoli pekee liliofungwa na Mzambia Davies Mwape lilitosha kutibua rekodi ya Simba ya kutofungwa katika ligi kuu ya Vodacom Tz.

Hongereni Yanga

Saturday, July 30, 2011

Yanga yaalikwa Sudan

Mabingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga itafanya ziara ya siku tano nchini Sudan ya Kaskazini tarehe 5 mwezi ujao ambapo inatarajiwa kucheza na vigogo wa soka wa nchi hiyo El Hilal and El Merreikh.

Huku mchezo wa ngao ya hisani dhidi ya Simba ukikaribia, mechi hizo mbili zitakuwa ni majaribio mazuri kwa Yanga kwa ajili ya kuanza msimu mpya wa ligi. Afisa Habari wa Yanga Louis Sendeu alisema jana kwamba Yanga imealikwa huko Sudan na klabu ya El Hilal.

El Hilal ambayo sasa inashiriki katika Ligi ya Mabingwa Afrika inanolewa na Kocha wa zamani wa Yanga, Milutin Srejdovic 'Micho'.

Monday, July 25, 2011

Ngao ya Hisani

Ngao ya Hisani yapigwa tarehe

Mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kufungua msimu wa Ligi Kuu ya Vodacom 2011/2012 kati ya Yanga na Simba iliyokuwa ichezwe Agosti 13 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, sasa itafanyika Agosti 17 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.

Uamuzi huo umetokana na timu ya Taifa (Taifa Stars) kuwa na mechi ya kirafiki katika kalenda ya FIFA (FIFA dates) ugenini itakayochezwa Agosti 10 mwaka huu dhidi ya Palestina. Stars itarejea nchini Agosti 11 mwaka huu baada ya mechi hiyo.

Wachezaji wengi wanaounda kikosi cha Taifa Stars kwa sasa wanatoka katika klabu hizo mbili. Awali Stars ilikuwa icheze mechi nyingine Agosti 13 mwaka huu jijini Amaan wakati aikitokea Palestina. Kocha Mkuu wa Stars, Jan Poulsen ameifuta mechi hiyo kwa vile Jordan haitakuwa na wachezaji wake wa kulipwa kutokana na kuwa nje ya kalenda ya FIFA.

Sunday, July 10, 2011

KAGAME CASTLE CUP

Fainali ya kufa mtu

Hatimaye fainali ya Kagame Castle cup ambayo ilikuwa ikisubiriwa na wengi inapigwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar kati ya Yanga na Simba.

Timu zote mbili zimeingia fainali baada ya kuvuka hatua ya nusu fainali kwa njia ya matuta. Simba iliitoa El Mereikh ya Sudan wakati Yanga iliitoa St. George ya Ethiopia.

Timu hizo mbili zinaingia zikitaka kulinda rekodi zake katika michuano hiyo:

YANGA:
Kocha Sam Timbe katika mechi zote tatu alizotinga fainali. Amefanya hivyo akiwa na SC Villa, Polisi za Uganda na Atraco ya Rwanda.

SIMBA:
Haijapoteza fainali yeyote ya Kagame iliyopigwa katika ardhi ya Tanzania. Tayari imefanya hivyo mara sita.

Mchezaji kwa uhakika atakosa mchezo wa leo kutokana na kadi ni Jerry Santo wa Simba ambaye ana kadi mbili za njano.

Bingwa wa michuano hiyo atajinyakulia dola za Kimarekani 30,000

Friday, July 08, 2011

KOMBE LA KAGAME

Yanga yatinga fainali

MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga imetinga katika fainali ya kombe la Kagame baada ya kuichapa St. George ya Ethiopia kwa mikwaju ya penati 5-4.

Timu hizo mbili zilishindwa kufungana katika dakika 90 na hata katika muda wa nyongeza wa dakika 30 bado mambo yalikuwa 0-0.

Penati za Yanga leo zilipigwa na:
Shadrack Nsajigwa (alikosa)
Nadir Haroub
Juma Seif
Davies Mwape
Hamis Kiiza
Nurdin Bakari

KOMBE LA KAGAME

Yanga vs St. George

MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga muda mfupi ujao inaingia uwanjani kupambana na St. George ya Ethiopia katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la Kagame itakayopigwa katika Uwanja wa Taifa.