Wednesday, October 10, 2007

MANJI: Nitarudi endapo.........

Wazee wa klabu ya Yanga jana walifanikiwa kumshawishi mfadhili mkuu wa klabu hiyo Yusuf Manji abadili msimamo wake wa kutoendelea kuifadhili timu hiyo.

Katika kikao cha wazee hao wakiongozwa na Yusuf Mzimba, Manji ameweka masharti ya kurejea na ufadhili wa klabu hiyo endapo uongozi wa sasa utatekeleza rasimu ya katiba ambayo imewaweka madarakani.

Moja ya mambo ambayo yameshindwa kutekelezwa hadi sasa ni zoezi zima la kuingiza wananchama wapya ambao wakiunganika na wale wa zamani watauziwa hisa na hivyo kuifanya klabu kuimarika kimapato na kujijengea misingi ya kujitegemea. Licha ya Manji kutoa hela kwa ajili ya shughuli hiyo, bado haijaanza.

Aidha Manji amesema hakuna kiongozi yeyote aliyemfuata kuhusu suala la yeye kuongeza mkataba wa ufadhili ambao uliisha tangu Septemba 30. Na baada ya kuona hakuna anayeuliza kuhusu kusaini mkataba mpya basi yeye akaamua akae pembeni.

Pia Manji aligusia suala la kocha ambapo alisema kwenye mkataba wake yeye anatakiwa kumlipa kocha lakini hadi sasa suala la kuletwa kwa kocha mpya limechukua muda mrefu.

Katika hatua nyingine, Manji alikubali ombi la wazee wa klabu hiyo la kuisaidia timu hiyo katika maandalizi ya pambano lake dhidi ya Simba hapo Oktoba 24. Wazee hao waliomba msaada wa shilingi milioni 10 lakini Manji akaahidi kutoa shilingi milioni 50 ambazo zitakabidhiwa kwa Katibu Mkuu Lucas Kisasa. Kati ya hizo milioni 50, wazee watapewa shilingi milioni 10 kwa ajili ya "shughuli za wazee" kwa ajili ya mechi hiyo.

Haya Manji ndiyo huyo amerudi kiaina na uongozi una mambo mengi ya kutekeleza. Tuombe usalama tu klabuni siku ya mkutano wa wanachama wiki ijayo.

Alamsiki.

No comments: