Tuesday, November 20, 2007

Makocha wapya wasaini Yanga
Hatimaye makocha Dusan Kondic na Spaso Sokolaviski kutoka Serbia jana walisaini mkataba wa miaka miwili kuinoa klabu ya Yanga katika michuano ya Ligi Kuu pamoja na ile ya Kimataifa.

Hafla hiyo ya utiaji saini wa mkataba huo iliyofanyika katika makao makuu ya klabu hiyo huko Jangwani pia ilishuhudia kuagwa kwa aliyekuwa kaimu kocha mkuu wa klabu hiyo Jack Chamangwana.

Makocha hao ambao watakuwa wakilipwa na mfadhili mkuu wa klabu hiyo Yusuf Manji, wataanza kwa kuinoa klabu hiyo kwa kuweka kambi nje ya Dar kwa mwezi mmoja na kisha wataondoka na wachezaji 18 watakaofanya vizuri katika kambi hiyo kwenda Ulaya kujinoa zaidi.


Naye Kondic, ambaye ana uzoefu mkubwa wa kufundisha barani Afrika, alimshukuru Manji kwa kufanikisha zoezi hilo na hatimaye kusaini mkataba wao, lakini akawataka wapenzi wa Yanga kuwa na subira ya mafanikio.

''Wapenzi wa Yanga wanatakiwa watupe muda ili tuweze kufanya kazi yetu kwa kuwa mafanikio hayafanani na chumvi ambayo ukiweka tu kwenye mboga, inakolea hapo hapo," alisema kocha huyo aliyekuwa akifundisha soka nchini Angola.

Makocha hao walikuja nchini kwa mazungumzo na mdhamini wa Yanga, Yusuf Manji takriban mwezi mmoja uliopita.


No comments: