Saturday, November 24, 2007

TFF yawarejesha akina Mourice Jangwani

Thomas Mourice: Inasemekana alirejea Miembeni ya Z'bar

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limewataka wachezaji wote waliosajiliwa kuchezea timu za Ligi Kuu Tanzania Bara wanapaswa kuendelea kuchezea timu walizosajili hata kama mikataba yao imeisha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana, na Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela, ilisema wachezaji wote walomaliza mikataba yao wanapaswa kuendelea kuchezea klabu walizosajiliwa kwa makubaliano yale yale ya mkataba ulioisha.

Mwakalebela alisema wachezaji hao watafanya hivyo hadi hapo ligi itakapomalizika kutokana na mabadiliko ya kalenda ya mashindano kwa kuwa msimu huo unaanza katikati ya mwaka.

" Tunajua mabadiliko haya yameleta athari kubwa katika maeneo kadhaa ya mpira kwa kuwa mikataba hiyo ni lazima itambuliwe na kusajiliwa na TFF," alisema Mwakalebela.

Alisema hata hivyo uamuzi wa TFF hautamzuia mchezaji yeyote kusajiliwa na timu nyingine baada ya klabu kufikia makubaliano kwa mujibu wa kanuni.

"Mikataba mingi ya wachezaji iliangiliwa wakati msimu ukianza mwanzoni mwa mwaka na kumalizika mwishoni mwa mwaka, hivyo ni lazima kila mtu atambue kuwa mabadiliko haya yameleta athari," alisema.

Alisema hatua hiyo bado itampa uhuru mchezaji kujiunga na klabu nyingine, lakini hataruhusiwa kufanya mazungumzo na kiongozi yeyote wa klabu kama ilivyoamriwa, ili kuepusha migogoro. Ligi itamalizika Aprili mwakani.

Wachezaji Amri Kiemba, Thomas Mourice na Edwin Mukenya wa Yanga wamegoma kusaini fomu za timu hiyo kwa ajili ya michuano ya Kombe la Shirikisho kwa madai mikataba yao na Yanga imeisha.

MAJIRA


No comments: