Wednesday, December 12, 2007

Hatma ya Mwalala leo

Uongozi wa Klabu ya soka ya Yanga umesema kuwa utatoa tamko leo kuhusu hatima ya mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya, Ben Mwalala, ambaye bado hajaripoti kambini jijini Mwanza.

Mchezaji huyo ameshindwa kuripoti kwenye kambi ya timu hiyo iliyo mjini Mwanza kujiandaa kwa michuano ya Kombe la Shirikisho la duru la pili la Ligi Kuu ya Bara, itakayokuwa mapema mwakani baada ya kushindwa kurejea kutoka kwao Kenya alikoenda mapumzikoni baada ya kumalizika kwa duru la kwanza la Ligi Kuu.

Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega alisema uongozi unasikitishwa na tabia hiyo iliyoonyeshwa na Mwalala wakati akijua ana mkataba na klabu hiyo ya Jangwani.

Kwa kweli Mwalala hana nidhamu, halafu msumbufu, uongozi umeshachoka na tabia zake, hivyo leo (jana) tunakutana kumjadili halafu tutatoa tamko kesho (leo), Madega, ambaye uongozi wake umeshawafungia kwa miezi sita wachezaji wake wawili Ivo Mapunda na Shadrack Nsajigwa- kwa kosa la kutoweka kambini mjini Morogoro na kumfungia miezi mitatu beki Edwin Mukenya aliyehamia Simba kwa kosa la kutoweka kambini siku moja kabla ya mechi.

Mwalala, pia alikuwemo katika orodha ya wachezaji waliotoweka kambini baada ya mechi na Simba, lakini hakuadhibiwa baada ya uongozi kuridhika kuwa kulikuwa na matatizo ya maelewano baina ya uongozi wa timu na Mkenya huyo.

Madega alisema kuwa Yanga imemvumilia Mwalala kwa kipindi kirefu, lakini imeonekana mpira umemshinda hivyo ni bora kuamua kumpoteza au kumpata.

Alisema uongozi ukimpigia simu kuhusu kuja nchini, amekuwa akitoa visingizio vingi ambavyo havina msingi wowote.

Kiongozi huyo alisisitiza kuwa hata kama Mwalala akiwa mchezaji mzuri, hana budi kufahamu kuwa nidhamu ina nafasi kubwa katika kikosi cha wanandinga wa klabu hiyo ya Twiga/Jangwani.

Mwalala aliuaga uongozi kuwa anaenda kwao Kenya kuoa na kwamba angerejea katika muda muhafaka, lakini hadi leo hajaripoti kambini.

Yanga, ambayo inafundishwa na kocha Mserbia Kondic Dusan, imeweka kambi ya wiki mbili mjini Mwanza na baadaye itahamishia kambi nchini Afrika Kusini hadi mapema mwakani itakaporejea tayari kwa Ligi Kuu na michuano ya Kombe la Shirikisho

MWANANCHI


2 comments:

Anonymous said...

Hamna lolote aibu tupu.Kuwaonea Ivo na Nsajigwa lakini kwa mtoto wao wa dhahabu hakuna kitakachotendeka.Sana sana ataambiwa awahi kambini.Kuwagawa wachezaji ndio maana hatuendelei.Au watasema wanajua tatizo lake.Madega najikosha baada ya wanachama wengi kumkalia rohoni.Wiki zaidi ya 3 mchezaji hujaripoti unataka nini???

Anonymous said...

Nilisema kabla kwamba ataambiwa awahi kambini.Kupewa siku 3 ndio nini??Ameshachelewa wiki tatu.Mwalala mvivu na sio mchezaji wa kulinda sheria.Kazi tunayo.Viongozi nao woga.Angekuwa mtanzania adhabu ingeshapita.