Monday, December 17, 2007

Kila la heri Said Maulid "SMG"

Winga machachari wa zamani wa Yanga, Said Maulid 'SMG' anastahili sifa kwa kuichezea Yanga kwa mafanikio makubwa tangu amejiunga nayo.

SMG ambaye ameuzwa kwa klabu ya Bravo du Marquiz inayocheza ligi kuu ya Angola Girabola, alijiunga na Yanga mwaka 2001 akitokea kwa watani zetu wa jadi Simba SC ambao nao walimtoa katika klabu ya Reli ya Kigoma.

Mchezaji huyo ameichezea timu ya Taifa ya Tanzania kwa vipindi tofauti kuanzia mwaka 2000 na moja ya mafanikio aliyoyapata ni kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa kombe la CECAFA Castle mwaka 2001.

Akiwa Jangwani amefanikiwa kutwaa mataji mbalimbali ya ubingwa wa ligi kuu ya bara 2002, 2005 na 2006. Pia ubingwa wa Muungano mwaka 2001.

Licha ya kuichezea Yanga kwa mafanikio, SMG aliwahi kuwekewa zengwe kwamba sio raia wa Tanzania siku moja tu kabla ya mechi ya Simba na Yanga. Hali iliyosababisha Yanga kugomea kucheza mechi hiyo hadi hapo serikali itakapotoa ufafanuzi ni kwa vipi mchezaji amewahi kuichezea timu ya Taifa anaambiwa sio raia na anatakiwa kuondoka nchini tena siku moja kabla ya mechi ya Simba na Yanga.

Mechi ambayo binafsi ninaikumbuka ni ile iliyochezwa huko Bulawayo mwaka 2001 dhidi ya Highlanders ya Zimbabwe katika mchezo wa ligi ya mabingwa Afrika - raundi ya kwanza ambapo SMG alikuwa mwiba mkali kwa ngome ya Highlanders kiasi cha kufunga mabao mawili na katika dakika za majeruhi aliangushwa ndani ya eneo la hatari lakini hata hivyo penati hiyo haikupigwa kutokana na mashabiki wa Highlanders kushikwa na hasira jinsi timu yao inavyochambuliwa nyumbani na mchezo huo ulivunjika Yanga ikiwa mbele kwa 2-0.

Kila la heri SMG huko uendako.

2 comments:

Anonymous said...

Nami namtakia kila la heri SMG.

Naomba kusoma kutoka kwako kuhusu timu ya watoto au reserve ya Yanga ile aliyokuwa anafundisha Chamangwana, inaendeleaje?

Anonymous said...

Kwa mujibu wa TFF, Yanga tayari imewasilisha majina 20 ya wachezaji wenye umri wa miaka 17 watakaochezea kikosi hicho.

Hata hivyo bado haijaeleweka programu ya mazoezi ya kocha ipo vipi.