Monday, April 28, 2008

Tumewakosa tena!

Mabingwa wapya wa soka wa Tanzania Bara, Yanga jana ilishindwa kuonyesha kuwa imepata dawa ya kumaliza `uteja` kwa mahasimu wao wa jadi, Simba na kukubali kutoka suluhu katika mchezo wa funga dimba wa ligi kuu ya Tanzania Bara iliyomalizika jana katika viwanja mbalimbali.

Kwa mara ya mwisho imeifunga Simba mwaka 2003, katika mchezo wa kirafiki uliochezwa mjini Mwanza, ambapo Yanga ilipata ushindi wa 3-0.

Katika kuonyesha kuwa Yanga haikuonyesha kuwa na njaa ya ushindi katika mchezo huo uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo timu hiyo kwa muda mrefu walicheza kwa tahadhari ya kutofungwa.

Dalili ya tahadhari za Yanga zilionekana hata pale Kocha wake, Dusan Kondic alipofanya mabadiliko kwa kumtoa mshambuliaji Maurice Sunguti na kumuingiza kiungo Credo Mwaipopo.

Tofauti na Simba iliiyoonyesha kupania ushindi licha ya kuwa na watu pungufu, ambapo Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic alimuingiza Athumani Machupa badala ya Mussa Hassan `Mgosi` na baadae kumwingiza Joseph Kaniki badala Ulimboka Mwakingwe.

Hata hivyo katika mchezo huo uliohudhuriwa na mashambiki wengi ulianza kuingiwa na kasoro baada ya mwamuzi msaidizi, Hamisi Chang`walu wa Dar es Salaam kukataa bao la wazi la Simba lililofungwa kwa kichwa na Emmanuel Gabriel katika dakika ya 27, hali iliyosababisha mwamuzi huyo kutupiwa chupa za maji na mashabiki.

Pia mwamuzi wa kati, Peter Mjaya kutoka Pwani naye alionyesha kushindwa kumudu mchezo huo kutokana na kutoa maamuzi ya kutatanisha ambapo katika dakika ya 82 alishindwa kuipatia Yanga penati baada ya mchezaji wake Credo Mwaipopo kuangushwa na Juma Nyosso.

Yanga, ambayo tayari ilikuwa imefanikiwa kutwaa ubingwa huo ikiwa na mechi tatu mkononi jana ilikabidhiwa Kombe la ubingwa mwakani itashiriki katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Kwa sare ya jana, Simba ilifikisha pointi 42 na kumaliza ligi hiyo ikiwa katika nafasi ya tatu na kukosa kushiriki katika mashindano ya kimataifa mwakani wakati Prisons ya Mbeya ndio imefanikiwa na kukata tiketi ya kushiriki katika michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kuilaza Polisi Morogoro 1-0 mjini Mbeya na kufikisha pointi 45.

Simba ndio walianza mchezo huo kwa kasi, ambapo katika dakika ya 20, beki wa Yanga, Nadir Haroub aliikosesha Simba bao baada ya kuutoa nje mpira uliopigwa na Moses Odhiambo wakati Mohammed Banka alipiga shuti safi katika dakika ya 32 lakini kipa wa Yanga, Benjamin Haule alilipangua.

Yanga nao katika dakika 24 walikosa bao baada ya kiungo wake, Amir Maftah kumlenga kipa wa Simba, Juma Kaseja huku akiwa amefanikiwa kumpiga tobo beki, Juma Nyoso na Ben Mwalala naye kupiga nje mpira katika dakika ya 63 huku akiwa amebaki peke yake na kipa Kaseja.

Odhiambo ambaye hucheza kwa kujiamini jana alipewa kadi nyekundu kufuatia faulo aliyomfanyia Mrisho Ngassa katika dakika ya 66 na hivyo kuifanya Simba kucheza pungufu.

IPPMEDIA

5 comments:

World of Soccer said...

Mechi ya Jumapili kama nilivyoiona.

Katika warm up kabla ya mechi ilionyesha wazi kabisa kwamba simba wataanza kipindi cha kwanza kwa mpira wa kasi. Walianza kwa kufanya warm up kwa mazoezi ambayo yanaongeza pace, Yanga wao walikuwa moderate.

Kipindi cha kwanza Simba walitawala kwa kuwa Yanga hawakufanya juhudi yoyote kuzuia uchezaji wa Simba.

Yanga ilicheza 3-5-2 wakati Simba walitumia 4-4-2. Kwa mitindo hii Yanga ilikuwa na watu wengi zaidi katikati wakati simba walikuwa na watu wengi pembeni. Ili Yanga iweze kuwaelemea simba ilitakiwa walazimishe mpira uchezwe katikati na sio pembeni, lakini katika kipindi hiki Yanga walitumia sana mipira ya pembeni kupitia kwa Ngasa. Mfumo wa 3-5-2 unaacha mashimo katika fullbacks hivyo kuwa rahisi kwa kina Odhiambo kuonekana wakicheza na kusumbua sana katika wings.

Yanga ilicheza na sweeper nyumba, kwa hiyo Yanga ilikuwa na mtu huru mmoja Nyuma. Simba hawakuwa na sweeper, Sweeper wao alikuwa Kaseja mipira yote iliyoanguka nyuma ya Mabeki alicheza yeye. Mtu huru wa kwao alikuwa Banka pale katikati na ndiye aliyekuwa mwiba wa mashambulizi kipindi cha kwanza. Maana ndiye aliyewachezesha wings na forward wa simba. Mipira yote iliyokuwa ikiokolewa toka golini kwa Yanga aliiokota yeye. Ili kumzuia huyu ilitakiwa kuasign mtu wa kucheza naye pale kati na kuforce kucheza kupitia katikati.

Kipindi cha pili nahisi ndio sababu ya Kondic kumtoa Sunguti na kumuingiza Credo na kumwambia Ngasa acheze na Mwalala pale kati. Japokuwa kwa muda fulani Ngasa alionekana kupotea na kurudi kucheza pembeni hadi pale Kondic alipomfokea.

kwa ujumla mechi kwa upande wa Yanga ilikosa utulivu. Kulikuwa na presha ya kuhitaji ushindi toka kwa pande zote.

Wachezaji,makocha viongozi, na hata mashabiki waliitaji ushindi kwa Yanga kwa sababu zao tofauti. Hii haikuwa nzuri kwa upande wa Yanga.

Regards

Tuntufye Abel
www.tuntucoach.blogspot.com

Anonymous said...

Asante saana kwa analysis yako. Imekaa vizuri.

Unaweza pia kutupa analysis ya ni wachezaji wa aina gani tunawahitaji ili tufanye vizuri CAF mwakani?

Mdau,

Anonymous said...

Mwanafyale,
Good analysis, hebu tupe ni wachezaji gani wamekuvutia toka ameingia Kodic

World of Soccer said...

Ni vigumu mno kusema wachezaji gani watafaa. Hii inatokana na mipango ya mwalimu mwenyewe na mfumo atakaotaka kuutumia kwa kipindi hicho. Kwa mfano kama Mwalimu ninaweza kuamua kuwa katika kila mchezo nitakaocheza ugenini, nitasimamisha striker mmoja na viungo watano na mabeki wanne. Nikiamua mfumo huu ina maana kuwa nitahitajika kuwa na striker mwenye mbio,pumzi, na pia awe na uwezo wa kukaa na mpira kwa muda mrefu bila kupoteza.

Kwa mantiki hiyo sitakuwa na uwezo wa kusema moja kwa moja kuwa ni wachezaji gani wanaifaa Yanga kwa ajili ya michezo ya CAF.

Lakini nikiwaangalia wachezaji wa Yanga waliocheza ligi msimu huu, ninaweza nikawaongelea baadhi tu.

1. Benjamini Haule: Licha ya kuwa hatulii sana golini na kuna wakati anapotea,pia kusumbuka sana katika kucheza krosi bado ni kipa mzuri. Ni mzuri kwa kuwa ana "determination" anapokuwa golini. Inawezekana udhaifu huu anaouonyesha sasa ni kutokana na kukaa benchi kwa muda mrefu hivyo kupoteza kujiamini. Akifanya mazoezi kurekebisha mapugufu haya bado ni kipa mzuri kwa kuwa ni mwepesi.

2. Nadir Haroub; huyu nampenda kwa kuwa ni mlinzi anayeamini katika "kufika"-Being first to the ball concept. Ingawa katika mechi na simba alionyesha kutokutulia (kila mtu anajua kuwa mechi Ya Simba na Yanga siku zote ina tension)bado ni beki anayefanya kazi kwa kujiamini na uhakika.

3. Credo Mwaipopo; Ingawa wengi wanalaumu uchezaji wake,kwa upande wangu bado naona ni kiungo mzuri. Credo hakai na mpira muda mrefu, ni mwepesi wa kutoa pasi na kwenda mbele kuipokea akiwa mtupu. Hii inaisaidia timu kwenda mbele kushambulia.

3. Athman Idd: Ana Ball control, ana Nguvu, ana Speed, Ni mzuri katika kupiga faulo, Pass zake za pembeni (Square pases) ni nzuri. Anahitajika kufanyia mazoezi kitu kimoja pass zake za kwenda mbele (penetrating passes), pasi nyigi za namna hii anazozitoa Chuji huwa zinapotea ajaribu kujifunza upigaji pasi hizi pamoja na zile ndefu za kuhama upande (kutoka kulia kwenda kushoto ama kutoka nyuma kushoto kwenda kulia).

4. Abdi Kassim: Nimzuri ila anahitajika afanyie kazi matumizi ya mguu wa kulia.

5.Mrisho Ngasa Ni mzuri sana bado mdogo hivyo ana nafasi kubwa tu ya kufanaya vizuri.

6. Vicent Barnabas ni mzuri ila tu anahitajika kujifunza kuinua macho anapokuwa na mpira. mazoezi ya kujifunza kuinua macho ni rahisi sana.

7. Jerry Tegete bado anafaa sana kwani bado mdogo hivyo ni rahisi kumpa vitu vipya ambavyo mwalimu atahitaji Jerry avifanye.

Kwa wale ambao hawakucheza msimu huu;

Yanga bado inamuhitaji Shadrack Nsajigwa; ni beki anayesaidia sana timu katika mashambulizi ya kutoka nyuma.

Umajeruhi wa James Chilapondwa ni pigo kubwa sana kwetu sisi wanayanga. Ni kiungo mzuri sana na anayejituma

Thanx

Tuntufye

Anonymous said...

Saafi,

Japo hukumwongelea Hamis Yusuf, nadhani naye anastahili kubaki kwa vile ana uwezo mkubwa kwa kukaba na kunyang'anya washambuliaji mipira. Anahitaji kufanyia kazi utoaji wake wa pasi ili ziwe na macho.

Mkongwe Sunguti pia nadhani apewe nafasi tena. Kina Tegete watajifunza mawili-matatu toka kwake.