Thursday, April 17, 2008

Ubingwa ni leo

YANGA leo inaweza kuwa na siku ya kumbukumbu ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom endapo itaweza kuishinda Ruvu JKT katika mchezo muhimu wa ligi hiyo.

Hata hivyo, ikishindwa kufanya hivyo timu hiyo italazimika kusubiri mchezo ambao utakuwa ukionyeshwa laivu kupitia televisheni ya GTV, Jumapili dhidi ya Prisons ili kuutwaa ubingwa huo msimu huu.

Lakini, ushindi dhidi ya maafande hao JKT Ruvu si rahisi kwani uzoefu unaonyesha kuwa zinapokutana timu hizo huwa na ushindani mkubwa.

Yanga, inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 46 kibindoni na endapo itashinda mchezo wa leo, itakuwa imefikisha pointi 49 ambazo kimahesabu haziwezi kufikiwa na timu yoyote nyingine katika ligi hiyo msimu huu.

Ikiwa chini ya Mserbia Dusan Kondic, Yanga inatarajiwa kushusha dimbani kikosi chake kamili ikifahamu kwamba kupoteza mchezo huo ni kujiweka mahali pabaya wakati ikisubiri mechi mbili muhimu dhidi ya Prisons na watani, Simba.

Prisons na Simba, ndizo timu pekee ambazo pia zina nafasi ya kutwaa ushindi wa pili na hivyo kuwa mwakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (Caf) mwakani.

Yanga ambayo ilikuwa na wachezaji sita kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichoshinda mabao 2-0 dhidi ya Harambee Stars ya Kenya, Jumamosi, leo haitegemei kupata mteremko kwa vijana wa Fred Felix Minziro, beki wa zamani wa timu hiyo. Timu hiyo imeonyesha uwezo mkubwa katika ligi hiyo.

Kocha Kondic atamkosa kiungo Athuman Idd aliyetolewa kwa kadi nyekundu dhidi ya Manyema FC wiki iliyopita.

Ushindi kwa Mserbia huyo itakuwa ni faraja ingawa ngome ya JKT Ruvu chini ya kipa namba mbili Stars, Shaabani Dihile inaweza kuichelewesha sherehe hiyo ya vijana wa Twiga/ Jangwani.

Kikosi cha Yanga kinaweza kuwa kile kilichocheza michezo mbali mbali ya ndani na ya kimataifa, ingawa faraja itakuwa kurejea kwa Mkongomani, Laurent Kabanda aliyekuwa majeruhi.

SOURCE: MWANANCHI

6 comments:

Anonymous said...

Tumalize mapema tujiweke sawa na watani wetu. mwaka huu hawachomoki

Anonymous said...

matokeo vipi jamaa bado? m sakran kuwait

Anonymous said...

jamaa vipi mbona kimya hivyo au kuna mvua huko?m sakran

CM said...

Yanga imelazimishwa sare ya 0-0.

Ubingwa bado.

Anonymous said...

sawa ni sehemu ya mchezo lakini mahesabu yanakuwa mazito maana kwa matokeo hayo wachezaji watakuwa katika mazingira mazito inshaallah mechi ijayo iwe ya ushindi

Anonymous said...

Hayo matokeo yana maana kuwa Yanga tayari ni bingwa, maana timu pekee yenye uwezo wa kufikisha point 47 ilizo nazo yanga ni Prison, huku Yanga ikiwa na goal difference nzuri zaidi ya Prison.

Ili Yanga ikose ubingwa inabidi ifungwe mechi zote 3 zilizobaki dhidi ya Prison, Kagera Sugar na Simba, tena ifungwe magoli mengi tuu, huku Prison nayo ikishinda mechi zake nayo kwa mgoli mengi.

Ktk hii scenario ni kwamba tunahitaji kuwapongeza vijana kwa kumaliza kazi mapema.