Monday, June 07, 2010

Uchaguzi Yanga Juni 27
UCHAGUZI Mkuu wa Yanga utafanyika Juni 27 mwaka huu. Uamuzi huo ulifikiwa jana katika mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika kwenye bwalo la maofisa wa Polisi Oysterbay Dar es Salaam.

Kupitishwa tarehe hiyo kunahitimisha muda wa uongozi uliopo madarakani chini ya uenyekiti wake Imani Madega na sasa klabu hiyo itaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Jaji John Mkwawa kwa kushirikiana na Katibu wa klabu hiyo Lawrence Mwalusako.

Awali katika mkutano huo Madega alipendekeza uchaguzi huo kuwa Julai 4, ambayo ilipingwa na wanachama wengi waliohudhuria mkutano huo, ambao walitaka uchaguzi huo ufanyike mapema zaidi.

Madega akitoa hoja ya kutetea tarehe hiyo ya uchaguzi iliyopangwa kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo alisema kwamba kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania, TFF ambayo Yanga ni mwanachama wake linatoa siku arobaini baada ya mkutano mkuu ndipo uchaguzi ufanyike.

Akizungumza baada ya Madega, Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani alisema chombo chenye maamuzi ya mwisho ndani ya Yanga kwa mujibu wa Katiba ya klabu hiyo ni mkutano mkuu.

Akifafanua zaidi Nyamlani alisema kwamba Katiba ya TFF ambayo Yanga imekubali kuiheshimu inatoa muda wa siku 40 za kufanyika kwa uchaguzi mara baada ya mkutano mkuu kukaa na kama mtu atataka kuongeza muda wa kukaa madarakani basi lazima apate ridhaa za mkutano huo.

Akizungumza huku akishangiliwa na wanachama 3133 waliohudhuria mkutano huo, Nyamlani alisema kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Yanga muda wa uongozi uliopo kukaa madarakani uliisha Mei 30 mwaka huu. Nyamlani alisema kwamba tayari TFF ilishatoa maagizo kwa uongozi wa Yanga ya kufanya marekebisho ya Katiba yao ndipo waendelee na taratibu za uchaguzi, huku wakizingatia kikomo cha muda wao wa kuongoza kwa mujibu wa Katiba yao ambao ni Mei 30 mwaka huu. Aliulaumu uongozi wa Yanga kwa kushindwa kufuata Katiba ya TFF na ile ya klabu yao, ambayo inaupa mamlaka ya mwisho mkutano mkuu wa kuamua mambo yao na sio Kamati ya Utendaji ya Yanga.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Mikataba na Hadhi ya Wachezaji wa TFF, Alex Mgongolwa akizungumza katika mkutano huo alisema kwamba Katiba ya Yanga ilikuwa na upungufu mchache sana, jambo ambalo kama lingeshughulikiwa kwa haraka lisingechukua hata dakika tano.
Mgongolwa alielezea mambo hayo kuwa ni kifungu kinachoelezea muda wa ukomo wa uongozi, ambacho wao walitaka kubaki kama kilivyo, wakaondoa idadi ya wanachama ili kuitisha mkutano mkuu kutoka theluthi mbili mpaka kuwa nusu theluthi na kuondoa mwanya kama akitokea kiongozi dikteta kuweza kuutumia na kipengele kinachotaka Baraza la Wadhamini wa klabu liwajibike kwa mkutano mkuu na sio Kamati ya Utendaji.

Mgongolwa alisema kwamba wao kama TFF hawawezi kukaa kimya, huku wakiona mambo hayaendi sawa na akasema katika mambo ambayo FIFA wanasisitiza ni wanachama wake kuwa na muundo wa uongozi unaoeleweka.

Baada ya hapo Madega alisimama tena na kusema kuwa wao kama uongozi wana budi kutii yote yaliyoamriwa na TFF na akauliza wanachama mnataka marekebisho ya Katiba yapite au yasipite, wanachama wakajibu kwa sauti ya juu,tunataka uchaguzi.

Madega akauliza kwa mara ya tatu masuala ya TFF yamepita au hayajapita wanachama wakasema yamepita kwa sauti ya pamoja ndipo Madega akaamua kufunga mkutano kwa maana ajenda kuu ya mkutano huo ni kupitisha marekebisho ya Katiba.

Baada ya Madega kufunga mkutano wanachama wakakataa maana walijua kuwa kama mkutano unafungwa na wao wamekubali kupitisha marekebisho ya Katiba, maana yake wamekubaliana na tarehe aliyoitangaza awali ya Julai 4 na wao walitaka mapema zaidi ya hapo.

Ndipo akasimama Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa klabu hiyo, Jaji mstaafu John Mkwawa aliyenusuru kuvunjika kwa mkutano huo pasipo kufikia muafaka na kusema kwamba matakwa ya wengi lazima yafuatwe.

Mkwawa alisema kwamba kwa uongozi uliopo madarakani ulimaliza muda wake Mei 30 mwaka huu akapendekeza tarehe ya uchaguzi kuwa Juni 27 uamuzi ambao ulipokewa kwa shangwe na wanachama waliofurika ukumbini humo.

Madega alikubali tarehe ya uchaguzi kama ilivyotangazwa na Jaji Mkwawa na akasema kwamba walikutana kwa ajili ya kupitisha marekebisho ya Katiba ambayo tayari yamepita.

SOURCE: HABARI Leo

2 comments:

Anonymous said...

madega amejidhalilisha.

Anonymous said...

madega amejidhalilisha.