Thursday, November 29, 2007

Kondic ataka Yanga iendeshwe kisasa

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mserbia, Dusan Kondic, amesema kama viongozi wa klabu hiyo wataendesha klabu hiyo kisasa, Yanga itapiga hatua kubwa kisoka na kiuchumi.

Dusan mwenye mkataba wa miaka miwili na Yanga, alisema hakuna njia ya mkato ya kuelekea kwenye mafanikio, bali ni klabu kuendeshwa kitaalamu.

Akizungumza makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mtaa wa Twiga na Jangwani, Kariakoo, jijini Dar es Salaam jana, Kondic alisema tangu afike, amejionea mengi katika Yanga.

Alisema kipindi cha mkataba wake, atajitahidi kushirikiana na viongozi wa klabu hiyo kuijenga Yanga itakayokuwa tishio kisoka na kiuchumi.

Kondic alisema kwa kuliona hilo, ndiyo maana kabla ya kuanza kwa mazoezi, wachezaji wote wamepimwa afya ili kuweka katika rekodi.

Alisema, baada ya kujua afya ya kila mchezaji, Yanga itaondoka leo kwenda jijini Mwanza kwa ajili ya kambi ya wiki mbili kujiandaa kwa Kombe la Shirikisho.

Alisema ikiwa mwanza, atafanya mawasiliano na timu kadhaa za Afrika Kusini kwa ajili ya kujipima nazo nguvu kabla ya kuanza kwa Kombe la Shirikisho.

Kuhusu timu, Kondic alisema timu yake inaundwa na wachezaji wenye vipaji na kama itasukwa vema, inaweza kupata mafanikio makubwa.

Alisema moja ya mikakati yake ni uwepo wa timu za vijana wa chini ya miaka 14, 17 na 21 ili kuzalisha vipaji vitakavyokuwa msaada kwa timu hiyo na taifa.

Alisema haandai Yanga kwa ajili ya kuifunga Simba, bali Yanga itakayokuwa ya ushindani wa kimataifa.

TZ DAIMA

No comments: