Wednesday, December 05, 2007

Ivo, Nsajigwa waomba radhi wanachama


Kipa namba moja wa Yanga, Ivo Mapunda na beki, Shadrack Nsajigwa wamewaomba msamaha wanachama wote wa klabu ya Yanga kutokana na makosa waliyofanya na kuwabembeleza viongozi wao wawarejeshe katika kikosi cha timu hiyo.

Wachezaji hao ambao walifungiwa kutokana na kuondoka kambini bila ya kutoa taarifa walisema hayo jana wakati wanazungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Shirikisho la soka nchini, (TFF).


Ivo alisema kuwa lengo la kuamua kuomba radhi ni kutokana na kuamini kuwa kosa walilofanya ni la kibinadamu na wao kama wachezaji wanategemea soka ili kujiendeshea maisha yao.


Alisema kuwa wamefikia maamuzi hayo kutokana na kufahamu kuwa wao ni sehemu ya maendeleo ya mpira hapa nchini na hivyo kutocheza kunawaathiri wao na nchi pia.


`Tunaomba msaada kwa wana- Yanga wote watusamehe makosa tuliyofanya, tuko hapa kwa ajili ya maendeleo,` alisema Ivo.
Aliongeza kuwa mbali na kuondoka kambini bila ya ruhusa hakuna jambo lingine walilolifanya ikiwemo tuhuma za kuihujumu timu yao katika mechi yao na watani, Simba ambayo ilimalizika kwa Yanga kufungwa bao 1-0.

Inawezekana mambo ya kuchukua fedha yalikuwepo lakini mimi binafsi sijawahi kupokea fedha kutoka kwa mtu yoyote, alisema Ivo na kuongeza kuwa hawakucheza chini ya kiwango kama inavyosemwa na baadhi ya wana-Yanga.

Aliongeza kuwa tayari wameshaandika barua kwa viongozi wao na wanasubiri maamuzi kutokana na maombi yao. Naye Nsajigwa alisema kuwa wameamua kuomba radhi wanachama wa Yanga kwa sababu soka ndio kitu wanachokitegemea na kosa walilofanya linaweza kusamehewa.

Wachezaji hao wamesimamishwa miezi sita na klabu yao na kufanya kuondolewa katika kikosi cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kinachojiandaa na mashindano ya kombe la Chalenji.
Hata hivyo, kuna taarifa kuwa viongozi wa TFF walikuwa wanawahitaji wachezaji hao katika kikosi cha bara na waliwashauri kuomba radhi ili wasamehewe.

NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

wasamehewe, tuandae timu kwa ajili ya mechi za CAF. Kila mtu ameshajua kosa lake. Hakuna sababu ya kuendelea kug'ang'ania adhabu zisizo na maslahi kwa yeyote.

Anonymous said...

Nawaomba uongozi Yanga ufikirie msamaha kwa hao wachezaji. Wameshajifunza na nina imani hawatarudia makosa!
-Mosonga