Sunday, April 20, 2008

Tukose na leo tena?

TIMU ya Yanga leo inajitupa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kumenyana na Prisons ya Mbeya katika mchezo mkali wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Mchezo huo ambao utaonyeshwa moja kwa moja na kampuni ya GTV unatarajia kukamilisha ubingwa wa Yanga au kuendelea kuchelewesha kujitangazia ubingwa wa ligi msimu huu. Bingwa wa Ligi Kuu atazawadiwa Sh milioni 50 kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo Kampuni ya Vodacom inayotoa milioni 35 na GTV dola za Marekani 12,000 (sawa na zaidi ya milioni 14). Mshindi wa pili atapata takribani Sh milioni 24 ikiwa ni Sh milioni 13 kutoka Vodacom na GTV Sh milioni 10, wakati mshindi wa tatu atajikusanyia Sh milioni 11 ambazo ni Sh milioni nane kutoka Vodacom na dola za Marekani 7,500 kutoka GTV.

Yanga kwa sasa ina pointi 47 ikiwa ni sita dhidi ya Prisons iliyo nafasi ya pili, baada ya kucheza michezo 23 na kushinda michezo 14 kutoka sare mara tano na kufungwa katika michezo minne. Prisons inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 41 kutokana na michezo 24 iliyocheza baada ya kushinda michezo 11, kutoka sare mara nane na kufungwa michezo mitano.

Yanga inayofundishwa na kocha Mserbia, Dusan Kondic inashuka dimbani ikihitaji sare ya aina yoyote ili itangazwe bingwa. Ilikuwa na nafasi ya kufanya hivyo katikati ya wiki, lakini imechelewa kutokana na sare ya bila kufungana dhidi ya JKT Ruvu katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja huo. Prisons inahitaji kushinda mchezo wa leo ili ifikishe pointi 44 na kusubiri kushinda mchezo wa mwisho dhidi ya Polisi Morogoro utakaofanyika Aprili 27 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya kwa mabao mengi na kuomba Yanga kupoteza michezo mingine miwili iliyosalia. Mchezo huo, unatarajia kuvuta hisia za wapenzi wa soka nchini kwani Prisons nayo inataka ushindi au sare ili kujihakikishia nafasi ya pili nafasi ambayo inawaniwa na Simba na Mtibwa Sugar.

Baada ya mchezo wa leo, Yanga inabakiwa na michezo miwili, kwani inahitaji kusafiri hadi Bukoba kumenyana na Kagera Sugar mchezo utakaofanyika Jumatano ijayo kabla ya kuja kumaliza ligi na watani wao wa jadi Simba Uwanja wa Taifa, Aprili 27.

10 comments:

Anonymous said...

Mambo vipi washkaji! Hivi hili game linachezwa saa ngapi leo? Unajua sisi tunaoishi mikoani inabidi tufuatilie katika TV nimesikia GTV wataonyesha moja kwa moja.
Kila la Kheri kwa wana Jangwani wote.

Anonymous said...

Yanga imepata bao ktk dk ya 8 kupitia kwa Maurice Sunguti.

Ni 1-0.

Anonymous said...

dk. 32, Prisons wamesawazisha kupitia kwa Godfrey Bonny.

1-1

Anonymous said...

dk 64; JERRY TEGETE ANAIPATIA YANGA BAO LA PILI.

TUNAONGOZA SASA 2-1

Anonymous said...

DK.77 Prisons wamerejesha bao kupitia kwa Godfrey Boniface.

Ni 2-2.

Anonymous said...

matokeo vipi? mpira bado unachezwa au ushakwisha?

Anonymous said...

Mpira Umekwisha 2-2.

Yanga imefikisha pointi 48 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yeyote.

Hata hivyo kuna habari kwamba Simba imekata rufaa katika Baraza la rufaa CAS ili irudishiwe pointi zake ilizopokwa dhidi ya Coastal Union hivyo bado wana matumaini ya kufikisha pointi 49 endapo itashinda mechi zake 2 zilizobaki.

Anonymous said...

muhimu tukishinda mechi ijayo hata kama watarudishiwa hizo point bado bingwa atakuwa yanga mpira ulikuwa mzuri vijana wamecheza vizuri m sakran kuwait

Anonymous said...

Ustaadh Sakran,

By the way, umeircord hiyo mechi? pili kama wamecheza vizuri tatizo lilikuwa wapi? mpaka Prison wakarudisha magoli au wamecheza kwa kuogopa? hivi mechi inayokuja tunacheza na nani?
From USA

Anonymous said...

samahani mimi sikuona huo mpira ila nimekosea kuweka alama ya kuuliza na mechi ijayo na kagera sugar ya bukoba lakini nina imani wamecheza kwa kujiamini zaidi kuwa tayari ni mabingwa hilo tatizo mara nyingi linawapata wachezaji wa timu nyingi ikiwa wanaimani ubingwa upo mikononi m sakran