Saturday, October 18, 2008

Kila la heri Ivo

"Kwaherini"

Hatimaye kipa wa kimataifa wa Yanga, Ivo Mapunda amefanikiwa azma yake ya kucheza soka ya kulipwa nchini Ethiopia akiwa na klabu ya St. George.

Klabu hiyo ya Ethiopia imekubali kutoa dola 8000 ambazo zilitakiwa na klabu yake ya zamani ya Yanga ili ikubali kumwachia. Awali St. George ilitoa 'ofa' ya dola 3000 tu ambazo zilikataliwa na Yanga.

Ivo alijiunga na Yanga mwishoni mwa mwaka 2005 akitokea Moro United na kabla ya kuidakia Moro, alikuwa akiidakia Prisons ya Mbeya.

Tangu mwishoni mwa mwaka jana, Ivo amekuwa katika hali ya misukosuko ndani ya klabu hiyo hali iliyoosababishwa na kufungwa bao pekee katika mechi dhidi ya Simba mwezi Oktoba mwaka jana. Mara baada ya mechi hiyo Ivo aliondoka kambini kuhofia kipigo kutoka mashabiki waliokuwa wakimtuhumu kuruhusu bao hilo kirahisi. Ivo alifungiwa kucheza soka miezi 6 na uongozi wa Yanga kwa kutoroka kambini usiku huo.

Hata hivyo licha ya misukosuko hiyo, mambo yake katika timu ya Taifa yamekuwa yakimnyookea kwani tangu kutua nchini kwa kocha Mbrazil Marcio Maximo, amekuwa akimchagua kama kipa namba moja wa timu hiyo. Hata hivyo katika kikosi kijacho Maximo atalazimika kuteua kipa mwingine kwani Ivo atakuwa amepoteza sifa za kuwemo katika kikosi cha taifa cha wachezaji wa ndani ya nchi.

Mbali ya Ivo, Yanga msimu huu imesajili makipa wengine 3 - Juma Kaseja, Obrev Circkovic na Steven Marashi.

Kila la heri Ivo katika maisha mapya huko St. George Ethiopia chini ya Milutin Srejodevic "Micho".

4 comments:

Anonymous said...

Misukosuko sehemu ya kazi ni jambo la kawaida.

Tunakutakia kila la heri Ivo, hko Ethiopia. Itumie hiyo nafasi kujitangaza zaidi hadi Ulaya.

Good luck,

Anonymous said...

Kwa umri alionao hawezi kugusa ulaya hata kama ni mzuri kiasi gani.
Kila raheri.

CM said...

Kipa wa timu ya Taifa ya Misri Essam El Hadary amepata timu huko Uswisi akiwa na umri wa miaka 35.

Anonymous said...

kila la kheri ,kule uendako tunakushukuru kwa kila kitu ,unategemea mpira kwa kuishi ,sisi mashabiki wengine hatujui undani wa maisha yako kwa hiyo asante sana .mtanzania mwenzako.