Wednesday, February 11, 2009

Taifa Stars vs Warriors

Mchezo wa Kimataifa wa kirafiki kati ya Taifa Stars na Warriors ya Zimbabwe unaendelea ndani ya Uwanja wa zamani wa Taifa.

3 comments:

CM said...

Dakika zilizoondoka hadi sasa ni 75 na bado mambo ni 0-0.

CM said...

Mpira umekwisha kwa sare ya 0-0.

Stars imeendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo wowote wa kirafiki nyumbani chini ya Marcio Maximo.

Anonymous said...

Jangwani ilivyo sasa

Jengo la klabu ya Yanga lililopo mitaa ya Jangwani kama linavyoonekana pichani likiendelea kufanyiwa ukarabati mkubwa.
Na Saleh Ally

KUNA uwezekano mkubwa baada ya miezi miwili ijayo, Yanga itakuwa ndio klabu yenye makao makuu bora zaidi kwa timu zote zilizo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kipindi hiki hasa zile zinazomilikiwa na wananchi na si makampuni au serikali.

Ukarabati unaoendelea katika makao makuu ya Yanga mtaa wa Jangwani na Twiga, Kariakoo jijini Dar es Salaam unaashiria kila sababu kwamba Yanga itaweka rekodi hiyo ya kumiliki jengo la kisasa lenye vyumba vya kulala 36, mgahawa, baa ndogo na chumba cha wazi cha mikutano chenye uwezo wa kuchukua watu wapatao 50.

Katika jengo hilo sehemu ya chini tayari umeanza ukarabati wa Uwanja wa Kaunda na Mwanaspoti ilishuhudia mafundi wakiwa katika hatua za awali kujenga mifereji ya pembeni ambayo itasaidia maji kutotuama kwenye nyasi iwapo mvua itanyesha. Lakini mafundi wengine walikuwa wanaendelea na ujenzi sehemu ya vyumbani, juu na chini ya jengo hilo.

Imeelezwa, tayari uongozi wa Yanga umethibitishiwa na mfadhili wao mkuu, Yusuf Maheboob Manji kufanyiwa ukarabati huo ikiwa ni pamoja na kuweka nyasi ingawa imeelezwa kulikuwa na majadiliano ambayo hayajafikia mwafaka iwapo ziwekwe nyasi bandia au za kawaida.

Katika ukarabati wa jengo hilo, mambo mengi yatakuwa mapya ikiwamo bwawa la kisasa la kuogelea ambalo wakati mwingine litakuwa linatumika kama sehemu ya kufanyia mazoezi kwa wachezaji wa timu hiyo.

Klabu nyingi hasa kutoka katika nchi zilizopiga hatua kubwa kisoka zimekuwa na makao makuu yenye vitu vingi vikiwamo viwanja na hosteli binafsi. Imeelezwa Jangwani wamekosa nafasi ya kujenga kiwanja kingine kwa ajili ya watoto na vijana kutokana na kuwa na nafasi finyu katika eneo hilo, hivyo timu zote zitalazimika kuchangia.

Ukiachana na hivyo, hivi karibuni ramani ya ukarabati huo ilibadilika na unaendelea kuinufaisha zaidi Yanga baada ya kuongezeka sehemu ya maegesho ya magari ya wachezaji na wageni watakaofika kwenye jengo hilo ambalo tayari limerudiwa kupakwa rangi za njano na kijani ambazo hutumiwa na timu hiyo.

Imeelezwa mabadiliko ya ramani hiyo yatafanya upande mmoja wa jengo hilo kuongezwa na Mwanaspoti ilishuhudia nguzo kadhaa zimeanza kujengwa kutokea chini upande wa magharibi wa jengo hilo la Yanga.

Mafundi walionekana wanaendelea na ujenzi sehemu mbalimbali za jengo hilo, kizuri zaidi au kama vile mshangao ukarabati wake ulionekana kuwa ni wa kiwango cha juu kwa kuwa kila chumba kimewekewa tiles na kiyoyozi (AC) huku bafu na vyoo vya kila chumba vikiwa vimejengwa kwa ubora wa juu, kukiwa na mikono ya mabomba ambayo wahusika wanaweza kuamua kutumia maji ya moto au ya baridi.

Kati ya timu ambazo zinaonyesha kuishi katika hali ya ubora kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni APR ya Rwanda na St George ya Ethiopia. Angalau Waethiopia hao wanatumia mali nyingi wanazomiliki kutokana na utajiri wao.

Lakini APR wamekuwa wakitumia vitu vingi vinavyomilikiwa na serikali kupitia Jeshi la Wazalendo la Rwanda chini ya Rais, Paul Kagame ambaye ni shabiki wao namba moja.

Mfano hosteli za timu ya taifa zilizo katika makao makuu ya Chama cha Soka Rwanda (Ferwafa) eneo la Remela na pia uwanja wa nyasi bandia ambao pia ni wa timu ya taifa ya Rwanda, Amavubi.

Hali kwa klabu nyingi za Uganda inaonekana kuwa si nzuri ingawa URA inayomilikiwa na mamlaka ya mapato inaonekana kuwa angalau. Maana yake, hata kama Yanga ingekuwa inazidiwa na timu kati ya URA na APR bado ingeendelea kuwa bora kwa kuwa hizo ni timu za mashirika wakati yenyewe ni timu iliyo mikononi mwa wananchi.

Imeelezwa kuwa makadirio ya ukarabati huo kukamilika ni ndani ya miezi miwili na baada ya hapo, kikosi cha Yanga kitaondoka katika hoteli ya Lamada na kuweka kambi katika makao makuu yao ikiwa ni sehemu ya kupunguza gharama.

Wakati Jangwani wakiwa wanasherekea neema hiyo, imeelezwa huenda Manji akaondoka na kuwaachia hiyo ikiwa ni zawadi yao ya karne ambayo pamoja na kupita wadhamini wengi katika klabu hiyo, hakuna ambaye amewahi kutoa zawadi kubwa kama hiyo kwa klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1935 na mwaka mmoja baadaye ikaanzishwa Simba ambayo jengo lake la makao makuu yake barabara ya Msimbazi jijini Dar es Salaam liko katika sura inayoonyesha huenda pia linasubiri mfadhili wa kulikomboa.