Saturday, May 16, 2009

Kondic kocha bora Tanzania 2008/09


Kocha Mkuu wa Yanga, Mserbia Profesa Dusan Kondic ametangazwa kuwa Kocha Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom 2008/09.

Pia klabu ya Yanga imekabidhiwa Sh milioni 37 kwa kuwa bingwa wa ligi hiyo, huku Simba ikipewa Sh milioni 14 kwa kushika nafasi ya pili na Mtibwa Sh milioni tisa kwa kushika nafasi ya tatu.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela alitangaza hayo wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa waliofanya vizuri katika ligi hiyo, ambapo walikabidhiwa hundi za fedha kulingana na zawadi zao zilivyo.

Mwakalebela alisema vigezo walivyotumia kumpata Kocha Bora, waliangalia muda aliokaa na timu, kama alifanya usajili na mafanikio yake, ambapo katika hilo Kondic pamoja an Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga walifuzu, lakini hatua ya mwisho Kondic aliibuka kidedea kutokana na mafanikio ya Yanga ambayo ni bingwa wa michuano hiyo. Mtibwa ilishika nafasi ya tatu.

Kondic alianza kuifundisha Yanga kuanzia mwishoni mwa mwaka 2007 akisaidiana na Mserbia mwenzake Spaso Sokolaviski. Kondic amekuwa akifanya vizuri katika soka la nyumbani lakini bado hajapata ufumbuzi wa tatizo linaloisumbua sana klabu hiyo la kutofanikiwa katika michuano ya kimataifa.