Friday, August 21, 2009

Suala la Owino

Rufaa ya Yanga yatupwa

KAMATI ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imetupilia mbali rufaa ya Yanga ya kupinga mchezaji wa kimataifa wa Kenya, George Owino, kuhesabiwa bado ni wake kwa msimu 2009/10.

Awali, Yanga ilipewa siku tano za kuacha mchezaji mmoja wa kigeni kati ya sita iliowasajili kwa msimu ujao wa Ligi Kuu inayoanza keshokutwa.

Hata hivyo, Yanga ilipinga agizo hilo na kuamua kukata rufaa kwa Kamati ya Mashindano, kwa hoja kuwa mchezaji mmoja anayezidi anaziba nafasi ya Owino aliyekwenda Ujerumani kwa majaribio.

Nyota sita waliosajiliwa msimu huu na Yanga, ni Jama Mba Robert, Steven Bengo, Moses Odhiambo, Kabongo Honore, Joseph Shikokoti na John Njoroge.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Florian Kaijage, baada ya Kamati ya Nidhamu kuijadili rufaa hiyo Agosti 19, ilibaini Owino bado ni mchezaji halali wa Yanga.

  • “Klabu ya Yanga ilikuwa na mkataba halali na mchezaji George Owino.
  • “TFF ilikwisha kutangaza kuhusu tarehe ya mwisho kwa timu zote kutangaza majina ya wachezaji watakaoachwa/ kusitishwa mikataba kwenye usajili wa msimu wa 2009/10, ambayo ilikuwa ni Juni 15.
  • “Klabu ya Yanga haikutangaza jina la mchezaji Owino kama mmoja wa wachezaji wa kuachwa.
  • “Suala la mchezaji kuruhusiwa kwenda kwenye majaribio kwenye klabu nyingine hakuwezi kumuondoa kwenye klabu yake ya awali hadi hapo taratibu za kumsajili kwenye klabu yake mpya zitakapokamilika, taratibu ambazo kwa upande wa mchezaji Owino bado hazijakamilika.
  • “Suala la kumsajili Owino kwenye dirisha dogo kama ilivyoelezwa na Yanga halina mantiki yoyote, kwani mpaka sasa Yanga imesajili wachezaji 10 wanaoruhusiwa, hivyo hakuna sababu ya kubahatisha kuwa timu itauza wachezaji wengine kupata nafasi yake,”

Kwa mazingira hayo, Kamati ya Nidhamu imesisitiza kuwa uamuzi wa Kamati ya Mashindano kuitaka Yanga kuondoa jina la mchezaji mmoja miongoni mwa wachezaji wapya wa kigeni ni sahihi.

Kwamba, Yanga inatakiwa kufanya hivyo ili kuingiza jina la Owino ambaye ni mchezaji wake halali kwa mujibu wa kanuni za ligi na mkataba baina ya Yanga na mchezaji husika.

Yanga imetakiwa kutomchezesha mchezaji yeyote mpya wa kigeni hadi pale imetamka ni mchezaji yupi anakatwa kati ya sita wapya, kabla ya mechi ya kesho dhidi ya African Lyon.

2 comments:

Anonymous said...

Waungwana tuna safari ndefu, nimeona wengi tunalaumu shirikisho , mimi binafsi pamoja na mapungufu yote na mapenzi yangu kwa Yanga. Naomba niseme uongozi wetu ni butu na ni dhaifu, kwa nini siku zote ytunataka kushindana na shirikisho? hivi kulikuwa na ugumu gani kwa yanga kutangaza majina ya wachezaji tutio wataka? kama tulikubali na kutia saini sasa leo tiunashindwa nini kumwambia mchezaji kuwa hatukuhitaji? achilia hilo mbali hivi si tulikuwa tunajua kuwa sheria ni kila timu iwe na watendaji nwaajiriwa sasa ni kwa nini tushindwe kufanya kwa wakati muafaka? Angalia pia hili la vitanda na TV kwenye vyumba kama Manji aliytoa pea sasa ni nanai kaiba hizi pesa? Manji ana kila halki kuitaka timu ikae Jangwani kama aliatoa pesa za kuifanya klabu iwe sawa na hoteli ya nyota tano. Ni jukumu letu wanachama kujiuliza tunakwenda wapi? kwangu inaonekana hata marehemu Mangara Tabu Mangara alikuwa mkweli na muwazi kuliko uchafu wa leo hii

Anonymous said...

Mdau, malalamiko yako ni ya msingi na kweli kuna tatizo la kiuongozi kwa kiasi fulani. Lakini ningependa kutofautiana nawe kwenye hili suala la Owino na taratibu za usajili kwa ujumla. Kama unakumbuka TFF walikuja na kauli ya kutaka vilabu vitangaze kuacha wachezaji wakati Yanga, kwa mfano, ilikuwa na wachezaji karibu 7 kwenye majaribio nje ya nchi. Hivyo Yanga hawakuwa wakijua ni yupi atafanikiwa na yupi atashindwa ili wasimwache. Kanuni ya TFF ni kama za FAT ile. Si, za kisasa kama FIFA inavyotaka. Nafikiri wajua kama hadi sasa bado vilabu duniani vinaendelea kusajili hadi Aug 31. Sisi ni kama tuna-operate dunia nyingine. Maana yake ni kwamba, zile timu za nje zilizowajaribu wachezaji wetu wakija leo na kusema basi tunawahitaji (maana usajili unaendelea duniani) then Yanga haiwezi kuziba nafasi zao hadi dirisha dogo (kama wanavyoita wenyewe TFF) mwezi Januari 2010. Hebu ona hilo tatizo. Mfano dhahiri utakaouelewa ni Nadir Cannavaro. Whitecaps wameamua kumsajili kuziba nafasi ya beki wao tegemeo waliyemtimua kwa ugomvi na mwenzake. La sivyo, ilikuwa Cannavaro arudi na Nizar tu ndio asajiliwe ka kuwa nafasi za wachezaji wa nje Whitecaps zilijaa. Je, Cannavaro angerudi angecheza Tanzania tena? Jibu ni hapana, kwani muda wa TFF kusajili ulishakwisha. Unaona tatizo lililopo? Ndio maana Yanga na wadau wanawataka TFF kubadili kanuni ziendane na FIFA kwa sasa mpira wetu si wa kienyeji tena.

Na TFF hawana kanuni mbadala ya kusema kwa kuwa Yanga wachezaji wa nje wamejaa, basi punguzeni mmoja mumkopeshe Moro United au Prisons au Mtibwa kwa msimu huu ili kuhakikisha wanawasaidia wachezaji. TFF haijali madhara ya mchezaji mmoja wa nje kukatwa akabaki anazagaa na maisha yake kisoka yakafa.

Tunahitaji kubadilika Yanga na TFF pia.
Geoff Mwambe
Mannheim, Germany