Wednesday, November 25, 2009

Papic arejea

Kocha wa Yanga Kostadin Papic amerejea na kuwahi mazoezi ya kwanza ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Bara kwenye uwanja wa Uhuru, jijini Dar es salaam.

Mserbia huyo aliondoka nchini kwenda kwao kwa ajili ya mapumziko ya siku saba ya mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu na amerejea mara moja kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Tusker na mzunguko wa pili wa ligi.

Papic amerejea akiwa amewautaka uongozi wa klabu hiyo kumchagulia kocha msaidizi mzawa ambaye amewahi kuichezea Yanga na ambaye pia ana cheti cha mafunzo ya awali ya ukocha, jambo ambalo msemaji wa klabu hiyo ya Jangwani Louis Sendeu, amesema kuwa wameyazingatia katika kuchagua majina yaliyopendekezwa kwa ajili ya mchakato wa kumchagua msaidizi huyo.

Kikosi cha Mserbia huyo kimepata nguvu mpya baada ya nyota wake Godfrey Bonny kusema kuwa yuko 'fiti' kuitumikia timu yake katika michuano ya Kombe la Tusker pamoja na michezo ya raundi ya pili ya Ligi Kuu baada ya kuwa nje ya dimba kwa zaidi ya wiki sita kutokana na kusumbuliwa na goti.

Akizungumza na jijini jana, Bonny alisema kuwa kwa kiasi kikubwa maumivu ya goti yaliyokuwa yakimsumbua yamepungua na hata daktari wake amempa nafasi ya kuanza mazoezi mepesi na wenzake.

"Nashukuru Mungu nimepata nafuu kubwa na nimeanza mazoezi mepesi, naamini baada ya wiki moja ama mbili nitakuwa nimerudi kwenye hali yangu ya kawaida na nitaweza kuitumikia timu yangu," alisema Bonny.

SOURCE: nipashe

2 comments:

Anonymous said...

Yanga ninawapenda sana, ila nawaomba mbadilishe rangi ya maandishi. Kwenye kurasa nyeupe rangi yetu ya njano, mtandaoni maneno hayaonekani kabisa. Tumieni japo rangi ya kijani badala ya rangi ya njano.

Ni matumaini yangu kuwa maoni yangu mtayafanyia kazi. Ahsanteni sana.

This Is Black=Blackmannen

Anonymous said...

Mtoto wa JK ndani ya kamati ya uchaguzi wa Yanga

KLABU ya Yanga imetangaza kamati ya watu watano akiwemo mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani Kikwete, ambao jukumu lao litakuwa kuratibu zoezi la uchaguzi wake unaotarajiwa kufanyika januari 3 hapo mwakani.

Kizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya klabu hiyo jana, Mwenyekiti wa Yanga , Iman Madega alisema kamati hiyo itaongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Jaji Mstaafu John Mkwawa.

Ukiacha Ridhiwan, Mkwawa ambaye katika uongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) awamu ya kwanza alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa atashirikiana na wajumbe wengne Ysuph Mzimba, mwanahabari mwandamizi Angetile Osiah na Philemon Ntahilaja.

“Kamati inaanza kufanya kazi kuanzia leo (jana),” alisema Madega na kuongeza kuwa kamati hiyo itatoa utaratimu mzima wa zoezi hilo kadili muda unavyokwenda.

Madega aliogeza kuwa kamati hiyo pia itashirikiana na kamati ya TFF inayoratibu masuala ya uchaguzi.

Pia katika zoezi hilo la uchaguzi linalosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa klabu ya Yanga, kutakuwa na mdahalo rasmi kwa wagombea utakaoandaliwa na kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari hapa nchini ili kuwapa fursa kunadi sera zao.