Saturday, July 24, 2010

Nchunga atangaza kamati
UONGOZI mpya wa klabu ya Yanga chini ya Mwenyekiti wake, Lloyd Nchunga, umepitisha jina la Francis Kifukwe, kuwa mjumbe wa Baraza la Wadhamini na kuteua wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji, akiwamo Mbaraka Igangula.

Kwa mujibu wa Nchunga, maamuzi hayo yalifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji iliyokutana juzi kujadili mambo kadha wa kadha ya klabu hiyo pamoja na kuteua kamati ndogo ndogo.

Nchunga alisema uteuzi huo umezingatia vigezo mbalimbali bila kujali tofauti za makundi yaliyokuwa yameibuliwa na harakati za kuwania uongozi wa klabu hiyo katika uchaguzi wa Julai 18.

Alisema wamefanya hivyo kwa lengo la kudumisha hali ya umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama kwa masilahi ya klabu hiyo.

Mbali ya Igangula, wengine walioteuliwa kwenye Kamati ya Utendaji ni Seif Ahmed Seif na Pascal Kihanga.

Kamati zilizoundwa ni Nidhamu, Fedha na Mipango, Ufundi, Mashindano na kamati mpya ya uratibu wa matawi.

Waliomo kwenye Kamati ya Nidhamu ni Mark Anthony (Mwenyekiti), Ishengoma (Makamu Mwenyekiti), Idrisa Ismail, Msafiri Mkeremi na Hafidh Ally.

Kamati ya Fedha na Mipango itakayokuwa chini ya Charles Mgondo, itakuwa na Salum Rupia (Makamu), Isaac Mazwile, Charles Palapala, David Mataka, Michael Malebo na Abel Mtaro.

Kamati ya Ufundi itakayoongozwa na Mohamed Bhinda, wengine ni Ally Mayai Tembele (Makamu), Sekilojo Chambua, Paul Malume, Edgar Chibura, Maneno Tamba na Abeid Abeid.

Seif Ahmed Seif atakuwa mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano huku Majid Seif akiwa makamu, wakishirikiana na Abdallah Binkreb, Mzamil Katunzi, Albert Marwa, Moses Katabaro na Lameck Nyambaya.

Nchunga alisema wameunda kamati mpya ya kuratibu shughuli za matawi, ambayo itakuwa chini ya uenyekiti wa Tito Osoro, Kibwana Matokeo (Makamu), Ali Kamtande, Theonest Rutashoborwa, Mzee Yussuf, Sarah Ramadhan na Athuman Fumo.

Aidha, Nchunga alisema kamati ya uchaguzi inabaki kama ilivyo, ambapo nafasi nyingine ikiwemo ya meneja, katibu mkuu wa kuajiriwa na msemaji, utaratibu wake utajulikana baadaye.

No comments: