Monday, January 24, 2011

Manji ajieleza kuhusu Mtemvu
MFADHILI wa Yanga, Yusuf Manji ameibuka na kutoa sababu za yeye kumteua Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu kuingia kwenye bodi ya wadhamini wa klabu hiyo.

Akizungumza na kituo cha Televisheni cha TBC, Manji alisema kabla ya Mtemvu kutangazwa kuwa mmoja wa wajumbe wa bodi ya wadhamini aliwasilisha hoja ya kutaka aongezwe mbunge mmoja na mfanyabiashara mmoja kwenye bodi ya wadhamini ya klabu hiyo katika kikao cha kamati ya utendaji kilichokaa Novemba 30, mwaka jana kwenye hoteli ya Lamada jijini Dar es Salaam

“Hayo yalikuwa ni maoni yangu baada ya kuona wenzetu wa Simba tayari wana watu wa kuwatetea na kuwatatulia matatizo yao kwa haraka pale watakapokwama, mwenyekiti wao Rage ni mbunge, wana watu wengi bungeni kama Mohamed Dewji, Idd Azan, Musa Hassan ‘Zungu’ Makongoro Mahanga, wote ni wa hapa Dar es Salaam Yanga wana nani?”alisema kwa kuhoji.

“Ndio maana nilimpendekeza Mtemvu kwa vile niliona ana vigezo vinavyostahili, Halima Mdee ni mpya sijui ana mapenzi na timu gani kati ya Simba au Yanga, kuna hati za kufuatilia ardhi kwa ajili ya ujenzi wa ule uwanja wetu umekwama kuendelea kujengwa kwa vile kuna watu wamevamia pale wanatakiwa waondolewa sasa nani atafuatilia ardhi.

“Yanga imekuwa ikihangaikia uwanja kila kukicha, lakini kama tuna mtu Mbunge akiungana na Mbunge wa Simba ni rahisi kukaa na Waziri mhusika wakatatuliwa tatizo lao kwa urahisi tofauti na mimi, lakini wao kama wanaona Mtemvu hafai basi watafute mbadala mimi simng’ang’anii,”alisisitiza.

“Mimi kumteua Mtemvu si kwa utashi wangu ni baada ya mwenyekiti Lloyd Nchunga kunipa idhini hiyo ya kumtafuta mtu ambaye namuona anafaa, lakini kwa vile hawamtaki tusilumbane kwa ajili ya masuala haya tukaipeleka Yanga kwenye migogoro isiyokuwa na maana mimi nawaomba watafute mbadala na hata kama wanataka na mimi niondoke nipo tayari kukaa pembeni na kuwaachia Yanga yao."

SOURCE - MWANANCHI

No comments: