Friday, January 21, 2011

Wanachama: Nchunga asimamishwe
HALI ya hewa ndani ya Yanga, imezidi kuchafuka baada ya uongozi wa matawi wa klabu hiyo kuiagiza Kamati ya Utendaji, imsimamishe haraka Mwenyekiti wao, Lloyd Nchunga mpaka utakapofanyika Mkutano Mkuu wa wanachama wote kuamua hatma yake.

Hatua hiyo imekuja baada ya jana uongozi huo kupata barua ambayo Nchunga, alimwandikia mmoja wa wajumbe wa bodi ya udhamini, Francis Kifukwe ikimuagiza atafute wajumbe 10 kwa ajili ya kufufua kampuni ya Yanga.

Wakizungumza Dar es Salaam jana Makao Makuu ya klabu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani, katika mkutano wao, uongozi huo chini ya Mwenyekiti wake Mohammed Msumi, uliiagiza Kamati ya Utendaji kutekeleza haraka agizo hilo.

"Huku tunakokwenda si pazuri hata kidogo, kwa kuwa tunauzwa bila kujielewa na ili kuinusuru hali hii tunaomba, Nchanga asiamishwe haraka mpaka utakapofanyika Mkutano Mkuu wa wanachama," alisema Msumi ambaye ni Mwenyekiti wa matawi.

Alisema maazimio hayo yamependekezwa na viongozi 84 wa matawi, ambao walihudhuria mkutano huo wa jana ulioanza saa nane mchana.

Msumi alisema katika barua hiyo ya Nchunga aliyomwandikia Kifukwe, atafute wajumbe hao ambao kila mmoja atakuwa na uwezo wa kuikopesha Yanga sh. milioni 50 kwa mwaka bila riba, klabu hiyo iwe na mtaji wa sh. milioni 500.

Barua hiyo ambayo nakala yake tunayo, ilieleza wajumbe hao 10 watafutwe haraka ili wafufue kampuni hiyo kwa lengo la kufanya biashara kwa kutumia nembo ya Yanga kwa kipindi cha miaka 10.

Ilieleza kuwa katika wajumbe hao kumi watamchagua Mwenyekiti wao, ambao watafanya biashara na Yanga kwa kipindi cha miaka mitatu, baada ya hapo watarudishiwa fedha yao waliyoitoa na klabu kurudi mikononi mwa wanachama na wakati huo Yanga tayari itakuwa na mtaji wake wa kutosha.

Katika mkutano huo wa viongozi wa matawi ulimtaka Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Lawrence Mwalusako awafafanulie kama Kamati ya Utendaji ilipitisha maamuzi hayo, lakini katibu huyo alidai kwamba yeye kwa mara ya kwanza barua hiyo aliiona katika kikao chama Kamati ya Utendaji kilichofanyika juzi.

"Mimi barua hii niliiona katika kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika jana, ambapo Mwenyekiti wetu Nchunga alitukabidhi na kamati iliamua lisifanyike jambo hili mpaka watakapopitia baadhi ya vifungu vya katiba," alisema Mwalusako.

Katika mkutano huo viongozi hao wa matawi ulipitia ajenda kuu tatu, ushiriki wa timu yao katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho (CAF) na mgongano wa viongozi na uvunjwaji wa katiba.
.

2 comments:

Anonymous said...

mnachagua vihiyo sasa hiyo kazi.heee bwana simba ile trip ya barazil imekufaa .duh tonge mdomoni kashindwa?

Anonymous said...

mnachagua vihiyo sasa hiyo kazi.heee bwana simba ile trip ya barazil imekufaa .duh tonge mdomoni kashindwa?