Tuesday, June 21, 2011

Yanga yatema nane

MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga wametangaza kuwaacha nyota nane kwenye usajili wake msimu huu wakiwemo Athuman Idd, Waghana wawili pamoja na kipa wa Mserbia.

Akizungumza jijini jana, Ofisa Habari wa Yanga, Luis Sendeu alisema kuwa uongozi wa klabu hiyo umefika hatua ya kuwaacha wachezaji hao katika usajili wake kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi yao kushuka kiwango na wengine kumaliza mikataba yao.

Wachezaji waliotemwa na timu hiyo ni pamoja na Yahaya Tumbo, Nelson Kimath, Nsa Job, Razack Khalfan, Izack Boakye, Ernest Boakye, Athuman Idd na Ivan Knezevic.

“Wachezaji hao ndio tuliowaacha katika usajili wetu wa mwaka huu, hii ni kutokana na baadhi yao kumaliza mikataba na wengine kushuka na uongozi kuamua kuvunja nao mkataba.

“Wachezaji ambao uongozi umevunja nao mkataba na kuwalipa haki zao zote ni pamoja na Nsa Job, Nelson Kimath na Yahaya Tumbo wakati Ernest Boakye na Isack Boakye, Athumani Idd, Ivan Knezevic na Razack Khalfan wao mikataba yao imemalizaka na uongozi ukaona hakuna haja ya kuendelea kuwanao,” alisema Sendeu.

Alisema pamoja na kutangaza kuwaacha wachezaji hao bado timu hiyo ipo katika harakati za kusaka saini na nyota wa zamani wa URA na timu ya Taifa ya Uganda, Hamis Kizza ambaye kwa sasa yupo jijini Dar es Salaam kwa mazungumzo.

Katika hatua nyingine, timu hiyo inaondoka leo kwenda mkoani Arusha kwa ajili ya mchezo wake wa kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya utakaofanyika mjini humo.

Sendeu alisema kuwa katika mchezo huo wanatarajia kuwatumia wachezaji wote waliowasajili sasa pamoja na wale wa kimataifa.

Source: MWANANCHI

2 comments:

Anonymous said...

Mdau habari?

Matokeo ya Yanga na Gor Mahia yalikuwaje?

Pia vipi hatma ya Asamoah, amesajiliwa tayari?

Naomba unisaidie majibu tafadhali.

Mdau, Canada.

Hassan Said said...

Kila la kheri kwa timu yetu ya yanga katika michuano ya Kagame na tudhihirishe kuwa sisi ni mabingwa halisi wa Tanzania viongozi tuepuke porojo tufanye kweli