Wednesday, March 28, 2007

Utetezi kuanza kwa Moro Utd

Kindumbwendumbwe cha ligi ya soka ya Tanzania bara kitaanza Aprili 14 mwaka huu kwa Yanga kuchuana na Moro united huko Arusha.

Ligi ya mwaka huu ambayo itachezwa kwa makundi ina makundi 3 ambayo itachezwa katika vituo vya Arusha, Dododma na Morogoro. Yanga ipo katika kundi A ambayo mechi zake zitakuwa huko Arusha.

Makundi ya ligi hiyo ndogo ya TFF yapo kama ifuatavyo:

Kundi A - Kituo cha Arusha: Yanga, Moro United, AFC na Polisi Morogoro

Kundi B - Kituo cha Mororgoro: Simba, Ashanti, Polisi Dodoma na Prisons

Kundi C - Kituo cha Dodoma: Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, JKT, Pan Africa na Ruvu Shooting Stars

Baada ya kumalizika hatua ya kwanza ya ligi ndogo, ligi hiyo itakuwa na hatua ya pili ambayo itakuwa na sehemu mbili.

Sehemu ya kwanza ya hatua hiyo ya pili itahusisha timu sita ambazo ni timu mbili zitakazoongoza kwenye makundi matatu.

Timu hizo sita zitagawanywa katika makundi mawili ya timu tatu kila moja na timu mbili zitakazoongoza makundi hayo mawili zitacheza mchezo mmoja wa fainali ambapo mshindi wa mchezo huo atatawazwa bingwa wa Tanzania Bara na hivyo kuiwakilisha nchi katika Ligi ya Mabingwa Afrika na mshindi wapili atawakilisha kwenye kombe la Shirikisho.

Sehemu ya pili itahusisha timu nne. Hizi ni timu mbili ambazo zitamaliza za mwisho kwenye makundi mawili ya `A' na `B' yenye timu nne kila moja pamoja na timu mbili zitakazomaliza zikiwa za mwisho katika kundi `C' lenye timu tano.

Miongoni mwa timu hizo nne, timu mbili zitakazomaliza zikiwa mwisho zitashuka daraja na kucheza ngazi ya Ligi ya Taifa ngazi Wilaya.

Makundi yote yatakuwa katika vituo na timu zote zitacheza mikondo miwili (zitarudiana) isipokuwa kwa mchezo wa fainali pekee ambao utakuwa mmoja.

Ligi hiyo ndogo hatua ya makundi A, B na C inatarajiwa kumalizika May 4.

No comments: