Wednesday, May 16, 2007

Kifukwe: Uongozi Yanga basi

Aliyekuwa Rais wa klabu ya Yanga katika uongozi uliopita, Francis Mponjoli Kifukwe ametangaza kutogombea nafasi yoyote katika uchaguzi ujao wa klabu hiyo.

Katika taarifa yake aliyoitoa jana kwa vyombo mbalimbali vya habari, Kifukwe amebainisha hilo baada ya kuona minong'ono kuhusu yeye imekuwa mingi hali ambayo ingeleta mifarakano katika kuelekea kwenye uchaguzi utakaofanyika Mei 26.

Kifukwe pia amewataka wana Yanga washikamane na kuijenga Yanga imara chini ya uongozi mpya utakaowekwa madarakani katika uchaguzi huo na pia amesema kuitumikia Yanga si lazima mtu uwe ndani ya uongozi.

Sehemu ya taarifa yake inasomeka “Nawapongeza wana Yanga kwa ushirikiano wanaoonyesha sasa kujenga Yanga moja imara. Silaha yetu kubwa kwa sasa ni muafaka wetu na nawaomba wana Yanga tuulinde. “Tofauti zetu ziwe za kujenga na kuleta maendeleo siyo kubomoa na kuturudisha nyuma tulikopita. Muda wa longolongo umepitwa na wakati. Tunahitaji watu watakaofanya kazi ili kuiletea Yanga maendeleo,”

“Kama mwenyezi Mungu ataniweka hai, basi siku ya uchaguzi nitakwenda kutimiza haki yangu kama mwanachama kwa kupiga kura nikizingatia sera na uwezo wa mgombea.”

Tunamshukuru Kifukwe kwa muda wake wote aliotumikia klabu ya Yanga. Hapana shaka ni mmoja wa viongozi wenye msimamo thabiti, asiyeyumbishwa hasa katika kipindi ambacho Yanga ilikuwa na migogoro mikubwa ya Kampuni vs Asili. Kila la heri katika kuitumikia Yanga nje ya uongozi.No comments: