Monday, June 04, 2007

TAIFA STARS SPECIAL:

Ghana 2008?

Kwanza napenda kuipongeza timu yetu ya taifa - Taifa Stars kwa mchezo mzuri dhidi ya Senegal katika mchezo wa Jumamosi iliyopita na kutoka sare 1-1 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.

Timu yetu imefanikiwa kuwabana Simba wa Teranga kiasi kwamba wamesawazisha bao ambalo kuna wanaoamini kwamba ni offside lakini mimi naona ni bao safi tu.

Kiuchezaji timu yetu imebadilika na sasa tunaweza kupambana hata na timu imara za Afrika hasa tunapokuwa nyumbani. Cha kuzingatia zaidi kwa sasa ni kupata uzoefu wa mechi za ugenini na kuimarisha safu yetu ya ushambuliaji.

Kwa hivi sasa tupo nafasi ya 3 kwenye kundi letu tukiwa na pointi 5 sawa na Msumbiji baada ya kuifunga Burkina Faso 3-0 huko Maputo jana. Ushidi wa Msumbiji umeongeza ushindani katika kundi hili, kwani endapo Taifa Stars ikifungwa na Burkina Faso katika mechi yake ijayo itajikuta ipo mkiani na hivyo kuweka matumaini yetu ya kwenda Ghana kuota mbawa.

Hata hivyo katika soka lolote linaweza kutokea. Lakini ni vizuri Watanzania ambao baada ya miaka mingi wameanza kuipenda timu yao, wakaanza kuondoa mawazo kwamba ni lazima timu hiyo iende Ghana mwakani. Ni kweli timu tuliyonayo ni nzuri lakini ndiyo kwanza tunaanza kuijenga, hivyo tujiwekee malengo ya muda mrefu kwa ajili ya soka la Tanzania ikizingatia kwamba timu yetu inaundwa na wachezaji wengi wenye umri unaoruhusu kucheza soka kwa zaidi ya miaka 5 ijayo.


Wadau mnasemaje kuhusu Taifa Stars?

No comments: