Saturday, July 21, 2007

Tusker Cup kupigwa Moro

Michuano ya mwaka huu ya Tusker Challenge cup iliyokuwa ipigwe kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam sasa imehamishiwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Shirikisho la Soka nchini, TFF limetangaza mabadiliko hayo kufuatia nyasi bandia zilizokuwa ziwekwe kwenye uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam kuchelewa kutoka bandarini.

Hata hivyo ratiba inabakia vile vile kama ilivyopangwa hapo awali.

Jumla ya timu sita zinatajiwa kuchuana kuwania sh. milioni 25. Timu hizo ni Yanga, Simba, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar kutoka Tanzania, Tusker ya Kenya na SC Villa ya Uganda.

...............Cannavaro, Abdi kukosekana

Wachezaji wawili wa Yanga Nadir Haroub 'Cannavaro' na Abdi Kassim 'Babbi' hawatakuwemo katika kikosi cha timu hiyo katika michuano ya Tusker.

Kukosekana kwa wachezaji hawa kunafuatia kuitwa kwao kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) kwa ajili ya ziara ya mazoezi huko Ujerumani.

Kukosekana kwa Cannavaro huenda kukatoa nafasi kwa beki Lulanga Mapunda ambaye hajachezeshwa kwenye ligi ndogo. Katika nafasi ya kiungo anayocheza Abdi Kassim, wapo wachezaji kadhaa katika nafasi hiyo akiwemo mchezaji mpya kutoka Burundi Gille Yusuph ambaye ameanza mazoezi na timu hiyo.

No comments: