Wednesday, August 29, 2007

Madega: Micho anatuumiza vichwa


Sakata la Kocha Mkuu wa Yanga Milutin Sredojevic 'Micho' kuchelewa kurudi kutoka Serbia limechukua sura mpya baada ya Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega kukiri kwamba suala la kocha huyo linawaumiza vichwa viongozi wa klabu hiyo.

Akizungumza katika mahojiano na redio moja Jijini Dar es Salaam jana, Madega amesema kwa sasa uongozi unafanya mawasiliano rasmi ya barua ili kumtaka aweke wazi hatma yake ya kurejea kufundisha klabu hiyo.

"Tunamwandikia barua halafu yeye anatakiwa kujibu ili tuweke rekodi zetu sawa" alisema Madega. Pia Madega alisema mawasiliano na Micho yamekuwa magumu kwani wakati mwingine hapatikani. Aidha Madega amesema watafanya juhudi zote ili kujua hatma ya kocha hiyo na hata ikiwezekana itatuma mtu aende Serbia kufuatilia suala hilo.

Kocha wa Yanga Micho aliondoka kwenda Serbia mara baada ya ligi ndogo ya TFF kumalizika akidai kwamba anakwenda kutibiwa na kila anapofanya mawasiliano na uongozi wa klabu anawaambia kwamba anaendelea na matibabu.

Kwa hivi sasa Yanga inafundishwa na kocha wa makipa Razak Siwa pamoja na kocha wa muda Ahmed Amasha katika mazoezi kwa ajili ya ligi kuu itakayoanza mwezi ujao. Siwa ndiye aliyeiongoza Yanga kutwaa kombe la Tusker mapema mwezi huu.

Tusubiri tuone, maana haya masuala yanapochukua muda mrefu wale mashabiki "wananchi" wataanza kukosa uvumilivu na wataanza kuhoji "kwani yeye ndiyo nani?".

Subira yavuta heri INGAWA PIA TUNAAMBIWA Chelewa chelewa utakuta mwana si wako.

3 comments:

Anonymous said...

Inawezekana mkataba aliosaini Micho una mapungufu ndiyo maana hawezi kuchukuliwa hatua.
Kwa haraka utaona kwamba huenda anawajibika kwa Yanga Kampuni ambayo kwa sasa haijaundwa.

Anonymous said...

Hivi na hili suala la Kampuni ktk Yanga likoje? Maana toka Uongozi mpya umeingia madarakani, halisikiki. Sasa hata kama angekuwa anawajibika kwa Kampuni, kwa nini hao wahusika wa Kampuni wasilimalize, kama kuna mawasiliano kati ya viongozi wa klabu na kampuni?

Anonymous said...

Ni vema uongozi umfuatilie tujue kama hana mpango wa kurudi ili tuanze kutafuta kocha mwingine mapema.