Friday, August 31, 2007

Wasso kumfuata Banka Msimbazi

Beki mahiri wa kushoto wa zamani wa klabu ya Yanga, Ramadhan Wasso Ramadhan huenda akavaa tena uzi mwekundu katika msimu ujao wa ligi baada ya kuachwa kimizengwe na Yanga mwanzoni mwa msimu uliopita.

Wasso ambaye kabla ya kujiunga na Yanga alitokea Simba, alikaririwa na Kipindi cha redio moja Jijini Dar es Salaam akikiri kufanya mazungumzo ya awali na klabu hiyo ili asajiliwe kuziba pengo la Nurdin Bakari ambaye huenda asicheze tena soka baada ya kugundulika na matatizo ya moyo.

Mara kadhaa wachezaji wa Yanga ambao huwa wanaachwa katika usajili wanahamia mtaa wa pili (Simba) kwa hasira lakini huko nako mambo yao huwa hayanyooki kama wanavyodhani.

Si dhambi kwa mchezaji kuhamia klabu pinzani, lakini ni bora mchezaji anapoachwa kwenye vilabu hivi vikubwa aende kwenye timu kama Mtibwa, Ashanti n.k ambako watapata nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.

Mchezaji wa mwisho kuhamia Simba akitokea Yanga ni Mohamed Banka ambaye hakutumika sana katika ligi ndogo ya TFF iliyomalizika hivi karibuni.


No comments: