Monday, October 15, 2007

'Chuji' nje miezi 3

Shirikisho la soka nchini TFF limemfungia kwa miezi 3 kiungo wa Yanga Athumani Iddi "Chuji" kwa utovu wa nidhamu.

Akisoma adhabu za wachezaji, viongozi na waamuzi zilizotolewa na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho hilo, Katibu Mkuu wa TFF Frederick Mwakalebela amesema Athumani Iddi amefungiwa kwa miezi mitatu kutokana na kosa la kumtolea lugha chafu mwamuzi wa mchezo kati ya Yanga na Coastal Union uliopigwa mwishoni mwa mwezi uliopita kwenye uwanja wa Mkwakwani huko Tanga.

"Kwa vile mchezaji huyu amekuwa akirudia vitendo vya utovu wa nidhamu mara kwa mara, basi adhabu yake imekuwa ya miezi mitatu" Hii ni mara ya pili kwa "Chuji" kupatikana na hatia katika kamati ya mashindano ya TFF, mwezi wa nane alifungiwa kucheza mechi sita za michuano ya Kombe la Tusker kutokana na utovu wa nidhamu.

2 comments:

Anonymous said...

Nadhani sasa ni wakati mzuri kwa Bwana mdogo Chuji kujiangalia mwenendo wake kwani anakoelekea si kuzuri. Hakika, kwa sasa hapa Tanzania hakuna kiungo anayezungusha vizuri kama yeye isipokuwa matendo yake yanakera. Tatizo hili pia lipo kwa Shadrack Nsajigwa. Sijui kwa nini wanashindwa kuelewa. Angalia kitendo alichofanya Chuji; mpira umekwisha unataka kumpiga refa, kwa faida ya nani? Hata kama alituuma! Shadrack naye anatumia muda mwingi uwanjani kulalamika na kuhamaki bila sababu za msingi. Alipata kadi ya kijinga sana Burkina Fasso. Na kuna siku pale Jamhuri alireremka kwenye gari na kumfukuza shabiki kiasi cha kuhatarisha maisha yake. Wangeweza kuwaiga Hamisi Yusuf, Abdi, Gulla, na Kiemba. Si rahisi kuwakuta wachezaji hawa wanafanya mambo ya kitoto.

Anonymous said...

Ni kweli Chuji inabidi ajirekebishe maana kwa kukosekana kwake kwa miezi 3 si tu itakuwa pigo kwa klabu, bali hata yeye mwenyewe kwani uwezekano wa kuitwa tena kwenye timu ya Taifa utakuwa mdogo.