Friday, October 12, 2007

Songombingo laendelea

Ule mvutano kati ya mfadhili wa zamani wa klabu ya Yanga na Mwenyekiti wa klabu hiyo Imani Madega umechukua sura mpya baada ya viongozi nane wa klabu hiyo kutamka kwamba wao hawahusiki na matamshi ya Madega.

Katika taarifa iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Yanga Lucas Kisasa, ilisema baadhi ya maneno na maelezo yaliyotolewa na kusambazwa kwenye vyombo vya habari na mwenyekiti huyo yameudhalilisha uongozi mzima wa Yanga na hayakustahili kutolewa na Madega ambaye walimuelezea kuwa ana dhamana kubwa ya kuiongoza Yanga.

Taarifa hiyo imeendelea kusomeka ''Wako baadhi ya wanachama na wazee wa Yanga ambao waliumizwa, kusononeka na kupata mfadhaiko mkubwa kutokana na maneno na matamshi hayo, kwa kuzingatia hili uongozi mzima wa Yanga tunawaomba radhi wanayanga wote na wazee wetu walioumizwa kwa maneno hayo.''

Katika hatua nyingine, wazee wa klabu ya Yanga wamesikitishwa na kauli ya Madega kwamba wao ni waroho na wasaliti. Wazee hao wamesema wao hawana tamko zaidi ya kuwataka wanachama wajitokeze kwa wingi katika mkutano wa utakaofanyika tarehe 16 Oktoba ili wamalize mvutano huu.

Siongezi neno hapo kwa vile sipendi mivutano.


No comments: