Friday, August 01, 2008

Yanga wamgeuzia kibao Tenga

VIONGOZI wa matawi ya Yanga wamemtaka Rais wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodgar Tenga kuomba radhi ikiwa ni pamoja na kumchukulia hatua Katibu wake, Nicholaus Musonye kwa kutoa lugha ya matusi dhidi ya klabu hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Matawi ya Yanga, Mohamed Msumi, alisema Tenga anatakiwa kufanya hivyo kutokana na Musonye ambaye ni Katibu Mkuu wa CECAFA kutoa lugha hiyo hadharani na si kuomba radhi kwao kama alivyodai katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Alisema Tenga akiwa Rais wa CECAFA alitakiwa kulaani kitendo cha Katibu wake kuitukana Yanga, lakini inashangaza kuona amekuwa kimya na kuipa klabu hiyo mzigo mkubwa wa adhabu na kuwa ukimya wake unaonesha ameafiki matusi hayo. Tenga pia ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Alisema pamoja na Tenga kuwaomba radhi Yanga, watalazimika kumfikisha Musonye kwenye vyombo vya sheria, ili ichukue mkondo wake ikiwa ni pamoja na kumtaka alipe fidia. Musonye alikaririwa juzi akiomba radhi kuwa maneno aliyotumia kwao Kenya ni lugha ya kawaida.

Akizungumzia adhabu ilizopewa Yanga kutokana na kushindwa kutokea uwanjani kucheza na Simba mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu Kombe la Kagame, Msumi alisema hawakubaliani na adhabu ya CECAFA inapingana na kanuni za shirikisho hilo inayosema timu inayoshindwa kutokea uwanjani inatakiwa irudishwe nyumbani.

Pia alisema Yanga haikuona sababu za TFF nayo kutoa adhabu, huku tayari CECAFA ikiwa tayari imeshatoa adhabu kwani waliotoa adhabu CECAFA wengi wao pia walikuwepo kwenye kutoa adhabu TFF.

Yanga imefungiwa na CECAFA kucheza mashindano yake kwa miaka mitatu, pia imetozwa faini ya dola 35,000, ambapo TFF nayo imeifungia miaka miwili kucheza mashindano ya kimataifa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela, alisema kinachotakiwa kufanywa na Yanga sasa ni kutekeleza adhabu yake na kuwa imetolewa kwa kufuata taratibu zote.

Alisema kutokana na hali hiyo TFF imefunga mjadala wa jambo hilo na kuitaka Yanga kujiandaa na Ligi Kuu.

SOURCE: MAJIRA

4 comments:

Anonymous said...

HUKUMU YA KONDOO NA HAKIMU NI FISI .

Anonymous said...

Yanga ina makosa kutopeleka timu uwanjani... na inastahili Adhabu kwa kosa hilo kama sheria za CECAFA zinavyosema......
ila unapofanya Kosa lolote kuna adhabu inayojulikana kuwa timu itapata na kila kitu kipo katika Katiba za vyama vinavyoongoza soka hata FIFA yeynyewe ina katiba yake timu isipokwenda uwanjani kuna adhabu iliyopangwa ambayo inajulikana....
Sasa Tukiwaachia TFF na CECAFA watoe adhabu wanavyoona hatutashangaa siku wakiamua KUIFUTA kabisa timu maana wanakuwa na uongozi usio na mipaka na maamuzi ya jazba yasiyofuata misingi yeyote ile ...,
Kila Kosa lina adhabu yake cha kujiuliza ni kuwa hii TFF wameitoa wapiiii? au ni njia ya kuwapatia SIMBA nafasi ya kushiriki michezo ya kimataifa?
TFF msijifanye mko juu ya sheria nyie wenyewe mko madarakani kufuata katiba yenu na sheria mlizojiwekea....

Anonymous said...

Hii ni sawa na mtoto kuangua maembe shambani kwa hakimu wa wilaya, kisha hakimu huyo akamhukumu mtoto kifungo cha maisha, ili kumfundisha yeye na watoto wengine!

Kweli mtoto ana kosa, lakini kosa la kuiba vitu kama maembe lazima liwepo kwenye kanuni za adhabu, bila hivyo tukiacha mahakimu na majaji watoe adhamu kulingana na 'ukubwa wa kosa' au 'aibu waliyopata' haitashangaza siku moja kusikia adhabu za vifo kwa vibaka wa simu!

Zack,

Anonymous said...

nawaomba vingozi waliotuangusha kwa hili wajiudhulu mbele ya wananchi na walipe fidia.