Saturday, February 27, 2010

LIGI YA MABINGWA AFRIKA

Yanga yatolewa

FC Lupopo wamefanikiwa kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifunga Yanga 1-0 huko Lubumbashi.

Bao pekee la mchezo huo lilifungwa kwa kichwa na Kayembe Muyaya katika dakika ya 76.

Yanga itarejea Dar keshokutwa mchana.

Ligi ya Mabingwa Afrika

Lupopo vs Yanga
Mabingwa wa soka Tanzania, Yanga leo inapeperusha bendera ya taifa huko Lumbumbashi DRC wakati itakapopambana na FC Lupopo ya huko kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Stade de Kenya jijini Lubumbashi.
Habari za hivi punde kutoka huko Lubumbashi zinaeleza kwamba Yanga imefanya mabadiliko ya kikosi chake kilichoanza katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita ambapo Kipa atakaa Obren Circkovic wakati George Owino atacheza beki namba nne huku Godfrey Bonny na Jerry Tegete wakianza.
List kamili:
1. Obren
2. Nsajigwa
3. Maftah
4. Owino
5. Nadir
6. Chuji.
7. Nurdin
8. Bonny
9. Tegete
10. Ngassa
11. Kiggi
Yanga inahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili isonge mbele kwenye michuano hiyo. Pambano hilo linatarajiwa kuanza saa kumi na nusu kwa saa za Afrika Mashariki.

Thursday, February 25, 2010

Yanga yatua Lubumbashi

Kikosi cha wachezaji 18 na viongozi 8 cha Yanga kimetua jijini Lumbumbashi tayari kwa mchezo wa marudiano wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya FC Lupopo.

Yanga imewasili nchini humo huku wachezaji wake wanne wakipatwa na balaa la kupotelewa na mabegi yao. Wachezaji waliopotelewa na mabegi yao ni Jerry Tegete, Boniface Ambani, Godfrey Bonny na Obren Circkovic.

Hali ya hewa huko Lubumbashi ambayo ilikuwa ikiripotiwa kwamba ni ya mvua kubwa imebadilika na kwa siku tatu sasa mvua haijanyesha jijini humo.

Kikosi kilichotua nchini humo ni makipa- Yaw Berko, Obren Curkovic, mabeki- Shadrack Nsajigwa, Amir Maftah,George Owino, Fred Mbuna, Nadir Haroub Cannavaro, Wisdom Ndhlovu.
Viungo ni - Athuman Idd 'Chuji', Kiggi Makassi, Godfrey Bonny. Washambuliaji ni, Mrisho Ngassa, Jerry Tegete, Shamte Ally, Steven Bengo na Boniface Ambani.

Monday, February 22, 2010

Yanga vs Toto Africa

Ligi Kuu ya Vodacom inaendelea tena leo katika uwanja wa Uhuru wakati mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga watakapowakaribisha Toto Africa ya Mwanza.

Yanga inatarajiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa Toto Africa kwani vijana hao wa Mwanza maarufu kama Wana-Kishamapanda wapo katika kampeni nzito ya kuhakikisha wanabaki katika ligi kuu msimu ujao. Katika mchezo wao wa mwisho, timu hiyo iliifunga Majimaji huko Songea 2-1 na hivyo kujiweka vizuri katika kampeni yake.

Yanga nayo leo itautumia mchezo huo kujipima kabla ya kukwea pipa kuelekea Lubumbashi DRC kurudiana na Lupopo FC mwishoni mwa wiki.

Tusubiri dk. 90.

Thursday, February 18, 2010

Yanga vs Kagera Sugar
Baada ya kuwakilisha taifa mwishoni ya mwa wiki, Yanga leo inaumana na Kagera Sugar kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom itakayopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru.

Wednesday, February 17, 2010

TFF imechangia kipigo - Yanga

SIKU chache baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-2 katika mchezo wa kwanza hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Saint Eloi Lupopo, klabu ya Yanga imesema kipigo hicho kimechangiwa na TFF.

Yanga inadai kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), halikusikia maombi yao wakati ikijiandaa kwa mchezo huo, hali ambayo ilimfanya Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic ashindwe kutekeleza baadhi ya mipango yake, hivyo kwa namna moja au nyingine kuvuruga maandalizi yao.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Loius Sendeu alisema waliiomba TFF iahirishe baadhi ya mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara wiki mbili zilizopita hasa mchezo wao na Mtibwa, ili wapate muda wa kujiandaa na kucheza mechi za kimataifa za kirafiki, lakini TFF ilikuwa kichwa ngumu, matokeo yake ilikuwa rahisi wapinzani wao kushuhudia mechi zao za ligi na pia baadhi ya wachezaji kupata majeraha.

Kwa mujibu wa Sendeu kama TFF ingekubali kuahirisha mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar Jumatatu wiki iliyopita, ingewasaidia kupata mechi za kujipima nguvu dhidi ya timu za ama Afrika Kusini au Zambia.

Alilalamika kwamba mechi yao na Mtibwa Sugar wachezaji walichoka, lakini pia wapinzani wao walituma mashushu jambo ambalo wanaliona liliwaathiri kwa namna moja au nyingine.

Hata hivyo Sendeu alisema bado hawajakata tamaa na wameiomba TFF iwaahirishie mechi yao dhidi ya Kagera Sugar inayotarajiwa kufanyika kesho ili wapate kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya URA ya Uganda Jumamosi, ingawa hakuna dalili ya kufanikiwa ombi lao, huku pia wakitaka wasicheze mechi ya ligi mpaka watakaporudi kutoka DRC.

Papic amekaririwa na baadhi ya vyombo habari akilalamika kuwa kufungwa kwa Yanga kunatokana na kutopata maandalizi ya kutosha hasa mechi za kirafiki za kimataifa.

Yanga Jumamosi ilikubali kipigo cha mabao 3-2 katika mchezo wa kwanza hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo ili isonge mbele italazimika kushinda mabao 2-0 katika mchezo wa marudiano utakaofanyika Februari 28 mwaka huu mjini Lubumbashi, DRC.

SOURCE: Habari LEO

Jama Mba arejea
Mshambuliaji wa Yanga, Mcameroon Robert Jama Mba, aliyekuwa nchini kwao kwa zaidi ya miezi miwili amewasili Dar es Salaam jana tayari kuichezea timu hiyo.
Mba ambaye hata hivyo hajasajiliwa kwa ajili ya michuano ya CAF, ameuambia uongozi kwamba kuchelewa kwake kunatokana na matatizo ya kifamilia.

Saturday, February 13, 2010

LIGI YA MABINGWA AFRIKA 2010

Yanga vs FC Lupopo

Safari ya wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika - Yanga inaanza leo kwa kupambana na timu ya FC Saint Eloi Lupopo ya DRC kwenye uwanja wa Taifa Dar.

Yanga inatakiwa ishinde mchezo wa leo ili kujiweka katika mazingira katika mchezo wa marudiano utakaopigwa huko Lubumbashi wiki mbili zijazo.
Mchezaji pekee ambaye ni majeruhi kwa upande wa Yanga ni winga Kabongo Honore ambaye alifanyiwa upasuaji wa goti mwanzoni mwa mwaka huu.

Kocha Kostadin Papic anatarajiwa kuteremsha kikosi chake kamili ambacho kimefanya vizuri katika mechi zake tano za mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Vodacom. Papic alifunga safari hadi Lubumbashi mwishoni mwa wiki iliyopita ili kusoma mfumo wa uchezaji wa timu hiyo ya DRC.
Kwa upande wao FC Lupopo wanadai wameisoma vizuri Yanga na walituma wawakilishi wao kuja kutazama mechi ya mwisho ya ligi dhidi ya Mtibwa Sugar ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa 3-1.

Tusubiri dakika 90 na kama kawaida tutafahamishana kinachoendelea kutoka uwanja wa Taifa.

Friday, February 12, 2010

Lupopo watua TZ

Wapinzani wa Yanga katika mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kesho, FC Lupopo, wamewasili jijini Dar es Salaam jana huku wakiahidi kucheza kufa na kupona.

Timu hiyo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, iliwasili majira ya saa 1:00 usiku jana na kupokewa na wadau mbalimbali wa soka nchini.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Erick Katenda, alisema kuwa wamekuja na kikosi cha wachezaji 18 -- wanane wakiwa ni wa kimataifa – mmoja kutoka katika nchi ya Ivory Coast, mwingine Cameroon, wawili Zambia na wanne Zimbabwe.

Katenda ambaye aliwasili nchini tangu Jumatatu, alisema kuwa alishuhudia mechi mbili za ligi kuu ya Tanzania Bara – ya Yanga dhidi ya Mtibwa na Simba dhidi ya Manyema – na kwamba kutokana na kiwango cha wapinzani wao Yanga, hawawezi kuwadharau.

Tutacheza kufa na kupona,” alisema Katenda wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mara baada ya kuwasili kwa timu yake.

Monday, February 08, 2010

Yanga vs Mtibwa Sugar
Harakati za ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom inaendelea tena leo kwenye Uwanja wa Uhru wakati Yanga itakapopambana na Mtibwa Sugar.

Yanga ambayo awali iliomba mchezo huo uahirishwe, sasa itautumia mchezo huo kama mazoezi kabla ya kupambana na FC Lupopo ya DRC mwishoni mwa wiki hii.

Yanga hadi sasa imejikusanyia jumla ya pointi 30 ikiwa ni pointi 10 nyuma ya wanaongoza ligi hiyo.

Wednesday, February 03, 2010

Ligi Kuu ya Vodacom

Shughuli kuendelea leo

Ligi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kuendelea leo katika viwanja mbali mbali. Michezo itakayopigwa leo ni:

Yanga vs JKT
Kagera Sugar vs Simba
Mtibwa vs Majimaji
Toto vs Manyema

Tuesday, February 02, 2010

Yanga yaomba kuahirisha mechi

Mabingwa wa soka nchini, Yanga, wameliandikia barua shirikisho la soka nchini, TFF, kuomba kusogezwa mbele kwa mechi yao ya Jumatatu ijayo dhidi ya Mtibwa ili ipate nafasi ya kufanya maandalizi ya mchezo wao wa Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya FC Saint Eloi Lupopo ya DRC utakaofanyika Februari 13.


Afisa Habari wa klabu , Luis Sendeu, alisema kuwa barua hiyo imepelekwa jana TFF na wameomba mechi hiyo dhidi ya Mtibwa ipangiwe tarehe nyingine yoyote baada ya kufanyika kwa mchezo huo wa klabu bingwa.


Aidha, Sendeu alisema timu hiyo imekosa mechi za kimataifa za kirafiki za kujiandaa na Ligi ya Klabu Bingwa kutokana na maombi wanayoyatuma kugonga mwamba kila mahala kutokana na nchi nyingi kuwa bado zinaendela na ligi kuu zao.