Saturday, November 13, 2010

Nembo ya Yanga kutumika kibiashara


UONGOZI wa klabu ya Yanga umepanga kukusanya Shilingi moja bilioni kwa mwaka kutokana na kuitangaza nembo yao ambayo tayari wameshatangaza zabuni kwa makampuni na wadau mbalimbali.

Mmoja kati ya watu ambao wamejitokeza kununua zabuni hiyo ni mdhamini wa klabu hiyo, Yusuf Manji ambaye tayari ameshaanza kulipia Shilingi12 milioni kila mwezi tangu Machi na kupewa kibali cha kuendesha televisheni na gazeti.

Hata hivyo, chanzo cha habari kutoka klabu hiyo kimeiambia Mwananchi kuwa mdhamini Manji tayari amesajili shuguli 16 tofauti ambazo zitatengenezwa na kuuzwa huku klabu ikipanga kupata kiasi hicho cha fedha.

" Hiyo ni nia ya dhati na klabu yetu, tayari imeshawekwa mikakati ya kuhakikisha klabu inanufaika na nembo yake, vitu vitakavyotengenezwa na kuuzwa ni skafu, kanga, tisheti, vitabu mbali mbali vya shule, majarida, kofia, mikoba ya shule, na vitu vingine,"alisema kiongozi huyo kwa sharti la kutotajwa jina.

"Unajua Yanga hivi sasa ina wanachama 10,000 lengo la mdhamini ni kuhakikisha tunafikia wanachama 100,000 na viti hivyo vikiuzwa klabu itanufaika na yeye atanufaika pia, klabu itakusanya zaidi ya bilioni moja kwa mwaka,"alisema

Katibu mkuu wa klabu hiyo, Lawrence Mwalusako alipoulizwa kuhusu maendeleo hayo alikiri kuwa mikakati hiyo ipo, na tayari makampuni manne zaidi yamejitokeza kununua nembo hiyo ambayo watashirikiana na Manji.

Hata hivyo, Mwalusako hakuwa tayari kuyataja makampuni hayo kwa maelezo kuwa bado wanapitia vigezo mbalimbali kabla ya kuyatangaza.

No comments: