Thursday, November 18, 2010

Papic kuondolewa?

>
MDHAMINI wa Yanga Yusuf Manji amemtwisha mzigo Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Davis Mosha kutafuta kocha atakayechukua nafasi ya Kostadin Papic atakapomaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu.

Habari za uhakika kutoka kwa uongozi wa Yanga zinadai, Manji amemtaka Mosha kufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na mjumbe wa Kamati ya Ufundi, Seif Ahmed.

Pia Manji inadaiwa amependekeza Mosha na mwenzake washughulikie suala la kumrudisha mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyeuzwa Azam kwa mkataba wa mwaka mmoja na kukamilisha usajili wa mchezaji Mghana Kenneth Asamoah.

“Manji ametuma taarifa yake kwa viongozi kwamba hayo ndio mapendekezo yake baada ya kuzungumza na wachezaji na kutoa maoni yao juu ya kocha na nini kiboreshwe kwenye timu,” alisema mtoa habari wetu.

Manji alikutana na wachezaji wa Yanga wiki mbili zilizopita na kuwataka kutoa maoni yao juu ya Papic baada ya kuwepo madai kwamba Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo haimtaki.

“Taarifa ya Manji kuja kwetu inasema alivyozungumza na wachezaji wameonesha kwamba wanamhitaji kocha na hivyo maamuzi yake ni kuwa amemuongezea mkataba wa mwaka mmoja ambao utakwisha mwishoni mwa msimu wa 2010/2011 na kipindi hicho Mosha ashughulikie suala la kumpata mbadala wa Papic,”alisema mtoa habari huyo.

Kuhusu Ngasa Yanga ilimuuza kwa Azam mwishoni mwa msimu uliopita, suala ambalo wanachama na mashabiki wengi walionekana kulipinga na kufanya iwe moja ya ajenda za kampeni kutoka kwa waliokuwa wakigombea uongozi Yanga katika uchaguzi mkuu uliofanyika Julai.

No comments: