Wednesday, January 05, 2011

Chuji: Nimebakiza miezi 2 Yanga

Athuman Iddi 'Chuji' alisema juzi kuwa hataongeza mkataba wa kuichezea klabu hiyo baada ya kumalizika mkataba wake miezi miwili ijayo.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam na kituo cha televisheni cha Clouds TV kupitia kipindi chake cha Sport bar, Chuji alisema kuwa amefikia uamuzi wa kutoongeza mkataba wa kuichezea klabu hiyo baada ya kuchoshwa na maneno ya uongo ambayo baadhi ya viongozi wa Yanga wamekuwa wakiyapeleka kwa kocha wake, Kostadin Papic.

"Kwa kweli niseme wazi kwamba sina raha Papic alipokuja tu hakuwa na tatizo, isipokuwa kuna baadhi ya viongozi(hakuwataja) ndio wamekuwa wanapeleka maneno ya uongo kwake kwamba mimi sina nidhamu.

"Watu hao hao ndio waliokuwa wanapinga ujio wangu Yanga wakati natokea Simba, hali hii imesababisha Papic hataki kabisa hata kuniona.

"Ninachosubiri sasa ni mkataba wangu uishe baada ya miezi miwili halafu baada ya hapo sitaongeza tena mwingine bali nitatafuta timu nyingine kama ni hapa nyumbani au nje na maisha yataendelea,"alisema Chuji.

Chuji, pia alitumia nafasi hiyo kuelezea tukio la kukorofishana na Papic wakati wa mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Uhuru hivi karibuni akisema alishangaa kocha huyo kususia wakati kitendo hicho hicho cha kutoka nje alichokifanya yeye alikifanya Shadrack Nsajigwa siku moja kabla ya tukio hilo.

"Unajua tatizo Papic ameshapandikizwa vitu ambavyo hata iweje anaona Chuji ni mtovu wa nidhamu, hebu fikiria siku ile mazoezini alisusa kuendelea baada ya mimi kutoka nje, lakini siku moja kabla Nsajigwa alifanya kitu hicho hicho, lakini hakuchukua uamuzi wowote.

Alipotafutwa na Mwananchi Papic alikanusha madai ya Chuji kwamba amekuwa akipelekewa maneno ya uongo na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo na kusisitiza kwamba kutokuwepo kwa kiungo huyo katika kikosi chake kwa sasa kunatokana na kuwa majeruhi.



6 comments:

Anonymous said...

taraaaaaa......klabu ya taaraabu inakuja .......

Anonymous said...

chuji nilikuona mwanza ukicheza na simba ,kweli unatakiwa ujirekebishe ,ulipewa kadi ya kizembe ,unaigharimu timu yako .that is not professionalism.badilika babu unazeeka.

Anonymous said...

mtabadili makocha hadi mwisho wa dunia tatizo mpaka sasa hamlijui poleni sana , hapo tatizo sio mwalimu, ni wachezaji vichwa msonge!!!!!! waoneni hao simba moto chini wanajituma zaidi,

Anonymous said...

kweli kabisa ndugu.

Anonymous said...

we chuji nenda! kabla baba yako hajazaliwa Yanga ilishakuwepo na ilishachukua ubingwa. tumechoka na tabia zako! maana kwa macho yetu wengine tumekuwa tunakuona ukiwa na Monja kwenye mambo yenu!

Kwendaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa! Yanga ipo na itaendelea kuwepo!

SHIKABWE MSAFIRI said...

HAKUNA CHA SIMBA KUJITUMA WALA NINI WACHEZAJI WA KIBONGO UWEZO WAO UMEISHIA HAPO WALIPO,TUACHE MAPENZI TUSEME UKWELI ILI WACHEZAJI WETU WABADILIKE SIO KUWAVIMBISHA VICHWA KWA SIFA ZA KIJINGA ZISIZOWASAIDIA.