Yanga kuishusha Prisons leo?
VILIO au vicheko vitakavyotawala leo katika majiji ya Mwanza na Mbeya baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa wakati timu za Toto African na Prisons zitapotupa karatazao za mwisho za kubaki Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara kwa msimu mwingine.
Mechi nyingi za leo zinachukuliwa kama za kukamilisha ratiba ya ligi kwa timu nyingi isipokuwa kwa Toto African, Prisons na Manyema ambapo ni klabu moja tu inayoweza kujinasua kutoka kwenye janga la kushuka daraja msimu huu baada ya Moro United kuaga mapema.
Maafande wa Prisons na Toto African wote wana jumla ya Pointi 20 kila mmoja huku Manyema Rangers ikiwa juu yao kwa tofauti ya pointi mbili zaidi. Manyema wenye kibarua kizito dhidi ya Azam watakuwa wakiomba Prisons na Toto zipoteze mechi zao ili ibaki kwenye ligi.
Prisons ikishinda itafikisha pointi 23 na itakuwa mbele ya Manyema yenye pointi 22 na Toto African pointi 20,hivyo Manyema na Toto kuungana na Moro yenye pointi 15 kushuka daraja.
Prisons watakuwa kwenye uwanja wa Sokoine kuikabili Yanga. Wakati Toto watakuwa ugenini mjini Bukoba kwenye Uwanja wa Kaitaba kuwakabili wenyeji Kagera Sugar wenye pointi 23 ambao matokeo mabaya ya mchezo huo yanaweza kuwashusha daraja.
Endapo timu hizi tatu za mwisho zote zikishinda kwenye michezo yao Toto itafikisha pointi 23 kama Prisons ikishinda, lakini Manyema Rangers watanusurika kushuka daraja kwa kufikisha pointi 25.
Lakini hali hiyo inaweza kuchukua sura mpya kama Toto wataiifunga Kagera Sugar, Manyema wakatoka suluhu na Azam, huku Prisons wakiichapa Yanga mabao mawili timu zote nne za mwisho zitafikisha pointi 23.
Kwa kuwa Toto imeshafunga mabao 23, Manyema 20, Prisons 18 wakati Kagera imeziona nyavu mara 14 tu.
Hapo ndipo Kagera Sugar na Manyema Rangers zitakapoungana na Moro United kushuka daraja kwa kutumia sheria ya mabao mengi ya kushinda katika kuamua.
MSIMAMO WA LIGI MSIMU WA 2009/10